
Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani Baba Mtakatifu Francis amefariki dunia leo asubuhi Aprili 21, 2025 akiwa na umri wa miaka 88.
Kifo chake kimethibitishwa na Vatican kupitia taarifa rasmi iliyotolewa na Kardinali Kevin Farrell, ambaye ameeleza kuwa Papa Francis amefariki dunia saa 1:35 asubuhi kwa saa za Roma, baada ya kuugua nimonia kali. Papa Francis, aliyezaliwa huko Buenos Aires, Argentina, alikuwa Papa wa kwanza kutoka Amerika ya Kusini na mwanachama wa kwanza wa Shirika la Yesu (Jesuit) kushika wadhifa huo.
Ameongoza Kanisa Katoliki kwa muda wa miaka 12, akijulikana kwa unyenyekevu wake, kujitolea kwa haki ya kijamii, na juhudi za kulifanya Kanisa kuwa jumuishi zaidi.
Alikuwa akisisitiza mazungumzo ya kidini, ulinzi wa mazingira, na kuwahudumia masikini na waliotengwa.
Katika wiki za mwisho za maisha yake, Papa Francis alikuwa akipambana na matatizo ya kiafya, ikiwa ni pamoja na nimonia na matatizo ya kupumua, yaliyomlazimu kulazwa katika Hospitali ya Gemelli mjini Roma.
Kwa sasa, maandalizi ya mazishi yanaendelea, na taarifa zaidi kuhusu ratiba ya misa za mazishi na mchakato wa kumchagua mrithi wake zinatarajiwa kutolewa na Vatican katika siku zijazo.
No comments:
Post a Comment