WAZIRI AWESO AMUAGIZA MKURUGENZI RUWASA KWENDA KONDOA KUHAKIKISHA MIRADI YA MAJI INAKAMILIKA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, April 18, 2025

WAZIRI AWESO AMUAGIZA MKURUGENZI RUWASA KWENDA KONDOA KUHAKIKISHA MIRADI YA MAJI INAKAMILIKA



Na Okuly Julius _ KONDOA


Waziri wa Maji, Mhe. Juma Aweso, amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwenda Wilayani Kondoa kuhakikisha miradi yote ya maji inakamilika kwa wakati ili wananchi wapate huduma ya maji safi na salama.

Aweso ametoa agizo hilo katika kata ya Itaswi, tarafa ya Pahi Wilayani Kondoa, mkoani Dodoma, alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa maji wa bwawa la Itaswi.

"Miradi mingi ya Kondoa haijakamilika, ipo nusu nusu. Watu wanateseka bila maji wakati fedha zimetolewa. Nakuagiza Mkurugenzi wa Mfuko wa Maji kuhakikisha mkandarasi wa bwawa la Itaswi analipwa shilingi milioni 700 zote, na kabla ya mwezi huu kuisha amaliziwe milioni 200 zilizobaki ili mradi ukamilike," alisema Aweso.

Amesema hawezi kuendelea kuvumilia hali ya kuzindua miradi inayotekelezwa na wafadhili kila mwaka, wakati miradi ya Serikali haikamiliki kutokana na usimamizi hafifu, wakandarasi kutolipwa kwa wakati au uzembe mwingine.

"Sioni fahari kuzindua miradi ya wafadhili wakati miradi ya Serikali inasuasua. Sitakubali wananchi wa Kondoa waendelee kukosa huduma ya maji safi na salama," alisisitiza.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Kondoa, Dkt. Ashatu Kijaji, amemuomba Waziri Aweso kusaidia kumaliza tatizo la maji kwa wananchi wa jimbo hilo, akieleza kuwa miradi ipo lakini wakandarasi wanashindwa kuikamilisha kutokana na uhaba wa fedha na hofu ya kutolipwa baada ya kazi.

Dkt. Kijaji amesema ndani ya miaka minne ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, jumla ya Shilingi Bilioni 19 zilitolewa kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maji katika jimbo la Kondoa, ikiwemo ujenzi wa Bwawa la Itaswi ambao umetengewa Shilingi Bilioni 5.8.

"Tuna miradi mingine kama wa Sangwa (bilioni 3.5) na Masawi (bilioni 1.9). Mheshimiwa Waziri, hapa hutaji milioni, unatamka bilioni; hizi ni fedha ambazo Dkt. Samia ametupatia kwa ajili ya miradi ya maji Kondoa," alieleza Dkt. Kijaji.

Ameongeza kuwa kama miradi hiyo ingetekelezwa kwa wakati, wananchi wa Kondoa wangekuwa tayari hata kutoa zawadi ya ng'ombe kwa Waziri Aweso, lakini kwa sasa hakuna hata mradi mmoja uliokamilika, hali inayowakatisha tamaa wananchi.

Kuhusu Bwawa la Itaswi, Dkt. Kijaji alisema lilipaswa kukamilika Septemba 20, 2024, lakini hadi sasa bado halijakamilika huku mkandarasi akiwa eneo la mradi bila fedha. Ameomba fedha zitolewe ili kukamilisha ujenzi huo kwani bwawa hilo ni muhimu kwa huduma ya maji, uvuvi, na kilimo kwa kata sita zinazolizunguka.

“Wavuvi wameacha kuvua, wakulima wa mboga mboga wameacha kulima, na wakazi wa Itaswi wanalazimika kununua mahitaji kutoka kata nyingine, jambo ambalo linaathiri afya na uchumi wa wananchi wetu,” alisema Dkt. Kijaji.

Amesema zaidi ya miradi tisa ya maji inayotekelezwa na Serikali katika Jimbo la Kondoa haijakamilika, licha ya kuanza utekelezaji wake miaka mitatu iliyopita, huku fedha zikiwa zimeshatengwa.

Dkt. Kijaji ameongeza kuwa tangu achaguliwe kuwa Mbunge wa Kondoa, visima vimeongezeka kutoka viwili hadi 126, lakini maendeleo hayo yote yametokana na msaada wa wafadhili.

No comments:

Post a Comment