
📌 Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia yapunguza gharama kwa nusu katika Magereza
Imeelezwa kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia imepunguza nusu ya gharama iliyokuwa inatumika katika kuandaa chakula cha wafungwa katika magereza.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Gereza Kuu la Lilungu, Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Magereza, Abdallah Missanga wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali (mstaafu), Jacob Kingu iliyolenga kukagua maendeleo ya miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika Mkoa wa Mtwara.
“Tangu tumeanza kutumia gesi kumekuwa na manufaa sana. Kwanza, hata afya za waliokuwa wanaandaa chakula cha wafungwa zimekuwa nzuri tofauti na hapo awali walipokuwa wanatumia kuni.
Pia, kwa kutumia nishati safi ya kupikia ya gesi, tumeweza kuokoa gharama karibia nusu. Wakati tunatumia kuni, tulikuwa tunatumia kati ya Shilingi Milioni 3 hadi Milioni 4 kwa mwezi, lakini kwa sasa tunatumia kati ya Shilingi Milioni 1.5 hadi 1.9 kwa mwezi,” amebainisha Mkuu huyo wa Gereza.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Kingu amelipongeza Gereza hilo kwa kutekeleza agizo la Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyeelekeza Taasisi zote zinahudumia watu zaidi ya 100 kuanza kutumia nishati safi na salama ya kupikia.
“Tumefurahishwa kuona maelekezo ambayo yalitolewa na Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan yanatekelezwa. Wizara ya Nishati kupitia taasisi zake mbalimbali ikiwamo Wakala wa Nishati Vijijini (REA) tunatekeleza maelekezo hayo pia,” amesema Mhe. Kingu.
Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa REA pia imesaini makubaliano na Jeshi la Magereza kuhakikisha askari magereza wanapata nishati safi za kupikia.
Mhe. Kingu amesema REA imefanikiwa kufunga mifumo ya nishati safi ya kupikia katika magereza zote 129 nchini, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo hayo ya Mhe. Rais na kuongeza kuwa, mradi kama huo wa kufunga mifumo ya nishati safi ya kupikia unatekelezwa katika Kambi mbalimbali za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Gereza Kuu la Lilungu lililoanzishwa mwaka 1952 lilianza kutumia gesi asilia kama nishati ya kupikia mwaka 2022 ambapo gesi hiyo ilifikishwa na Shirika la TPDC.
















No comments:
Post a Comment