MAVUNDE AWATAKA WANAUSHIRIKA KUCHANGAMKIA FURSA ZA KIUCHUMI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, May 16, 2025

MAVUNDE AWATAKA WANAUSHIRIKA KUCHANGAMKIA FURSA ZA KIUCHUMI


Na Edward Winchislaus _ DODOMA 


Waziri wa Madini na Mbunge wa Dodoma Mjini, Mhe. Anthony Mavunde, amewataka wanachama wa vyama vya ushirika katika Mkoa wa Dodoma kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo mkoani humo ili kukuza na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi kupitia ushirika.

Mhe. Mavunde ametoa wito huo leo, Mei 16, 2025, alipokuwa mgeni rasmi katika kilele cha Wiki ya Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika Mkoa wa Dodoma. Amesema kuwa kutokana na ukuaji wa kasi wa kiuchumi wa mkoa huo, Dodoma imeendelea kuwa kitovu cha fursa nyingi nchini, hivyo kuwa na nafasi kubwa kwa vyama vya ushirika kushiriki kikamilifu katika kuziendea.

“Niwaombe wanaushirika wote kupitia jukwaa hili, tuangalie kwa makini jamii yetu ya Dodoma. Tumebarikiwa kuwa na shughuli nyingi za kiuchumi zinazoendelea. Natamani kuona vyama vya ushirika vikichangamkia fursa zinazopatikana, maana jiji letu linakua kwa kasi kubwa sana kiuchumi,” alisema Mhe. Mavunde.

Ameongeza kuwa vyama vya ushirika vinaweza kuwekeza kwenye mashamba makubwa ya kulima nyasi kwa ajili ya malisho ya mifugo kama ng’ombe, jambo litakalosaidia kukuza mifugo, kuongeza uzalishaji wa maziwa, na kuwafanya wanachama kuwa sehemu ya suluhisho la mahitaji ya chakula cha mifugo mkoani Dodoma.

Aidha, Waziri Mavunde amesema kuwa Serikali ina mkakati wa kujenga viwanda vikubwa saba vya kuchakata dhahabu katika mkoa wa Dodoma kutokana na rasilimali za madini zilizopo, na amewahimiza wanaushirika kushiriki kikamilifu ili wawe miongoni mwa watakaonufaika na miradi hiyo mikubwa ya kitaifa.

Kwa upande wake, Kaimu Naibu Mrajisi wa Uhamasishaji kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Bi. Consorata Kiluma, amesema tume hiyo inahakikisha kuwa vyama vya ushirika vinajiendesha kwa misingi ya kibiashara kwa lengo la kupata faida itakayowanufaisha wanachama.

“Tume inaendelea kuvisimamia na kuhamasisha vyama vyake kuwa imara kwa kuboresha kanuni, sheria na kuhakikisha vinaendeshwa kwa misingi ya kibiashara,” alisema Bi. Kiluma.

Awali, Mwenyekiti wa Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika Mkoa wa Dodoma, Bw. Ibrahim Ezakiel, akisoma risala kwa mgeni rasmi, alisema pamoja na mafanikio mbalimbali yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa jukwaa hilo, bado wanakumbwa na changamoto kadhaa, ikiwemo ukosefu wa maabara ya kupima ubora wa mchuzi wa zabibu – jambo linalosababisha uzalishaji usio wa viwango vya juu.

Maadhimisho ya kilele cha wiki ya Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika mwaka 2025 yamehitimishwa kwa kaulimbiu isemayo: “Ushirika Hujenga Ulimwengu Ulio Bora.”

No comments:

Post a Comment