Na Angela Msimbira, Pwani
Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Albert Msovela, amewataka Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ushirikiano na mshikamano ili kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Mikoa yao.
Akizungumza leo Mei 20, 2025, katika mafunzo ya uongozi kwa Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa yanayofanyika katika Chuo cha Uongozi mkoani Pwani, Msovela amesema kuwa ushirikiano ni nguzo muhimu katika kufanikisha malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwaletea wananchi maendeleo ya haraka na yenye tija.
“Ni muhimu tufanye kazi kama timu moja. Miradi ya maendeleo haiwezi kutekelezwa kwa ufanisi ikiwa kila mmoja atafanya kazi kivyake. Ushirikiano, mawasiliano na uwajibikaji ni mambo ya msingi,” amesisitiza Msovela.
Aidha, ameongeza kuwa Makatibu Tawala Wasaidizi wanapaswa kuratibu kwa ufanisi shughuli zote za maendeleo, kufuatilia utekelezaji wake kwa karibu na kutoa taarifa sahihi kwa wakati ili kuisaidia Serikali kufanya maamuzi yenye tija.
Msovela amesema viongozi hao ni kiungo muhimu kati ya wananchi na Serikali, hivyo ni lazima wawe karibu na wananchi, kusikiliza changamoto zao na kushirikiana nao katika kuzitafutia suluhisho la kudumu.
No comments:
Post a Comment