TANZANIA YANG’ARA KATIKA MKUTANO WA WAKAGUZI WA MAJITAKA MIGODINI NCHINI SWEDEN - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, May 20, 2025

TANZANIA YANG’ARA KATIKA MKUTANO WA WAKAGUZI WA MAJITAKA MIGODINI NCHINI SWEDEN


Na Mwandishi Wetu _ Sweden


Tanzania imeendelea kung’ara katika majukwaa ya kimataifa baada ya kuwa kivutio kikubwa katika mkutano wa Tathmini ya Mafunzo ya Ukaguzi wa Majitaka ya Migodini unaofanyika katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Luleå, nchini Sweden.

Mkutano huo wa kitaalamu unahusisha nchi saba zikiwemo Tanzania, Kenya, Liberia, Rwanda, Ethiopia, Zambia na mwenyeji Sweden, unalenga kuchambua na kuakisi mafanikio na changamoto za utekelezaji wa ukaguzi wa majitaka kwenye migodi kwa kutumia mbinu rafiki kwa mazingira na zinazozingatia maendeleo endelevu.


Kamishna wa Madini, Dkt. AbdulRahman Mwanga, anaongoza ujumbe wa Tanzania wenye wataalam 11 wakiwemo kutoka Wizara ya Madini, Tume ya Madini na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Katika moja ya vipindi muhimu vya mkutano huo, Tanzania iliwasilisha mada maalum tarehe 19 Mei 2025, ambapo ilieleza kwa kina fursa kubwa za uwekezaji katika uongezaji thamani madini, utafiti wa madini mkakati, na mikakati ya kuwajengea uwezo wataalamu wa ndani ili kukuza uchumi wa madini unaojali mazingira.

Wajumbe walioshiriki walionesha kuvutiwa na hatua zinazochukuliwa na Tanzania katika kusimamia rasilimali zake kwa uwazi, uwajibikaji na kwa kuzingatia maendeleo jumuishi kwa wananchi.

Tangu mwaka 2018 hadi sasa, jumla ya wataalam 54 kutoka Tanzania wamenufaika na mafunzo hayo, yaliyofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Sweden (Sida) kupitia ushirikiano wa Taasisi ya Jiolojia ya Sweden (SGU), Chuo Kikuu cha Luleå na Taasisi ya Mazingira ya Sweden (SEPA).

Mkutano huo unatarajiwa kufungwa rasmi tarehe 28 Mei 2025, ambapo washiriki watapata fursa ya kutembelea migodi mikubwa nchini Sweden ili kujifunza kwa vitendo kuhusu mifumo ya kisasa ya uendeshaji wa shughuli za migodi kwa njia endelevu.

Hatua hiyo ni ishara ya Tanzania kuendelea kuaminiwa na kushirikishwa kimataifa katika mijadala muhimu kuhusu usimamizi wa rasilimali za madini, huku ikijijengea mazingira bora ya kupokea wawekezaji wanaothamini maendeleo ya kweli na hifadhi ya mazingira.

No comments:

Post a Comment