PPRA, WEDAC WAWAJENGEA UWEZO WANAWAKE WAJASIRIAMALI HANANG KUPATA FURSA ZA KIUCHUMI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, May 4, 2025

PPRA, WEDAC WAWAJENGEA UWEZO WANAWAKE WAJASIRIAMALI HANANG KUPATA FURSA ZA KIUCHUMI



Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Aprili 29, 2025 imeshiriki tukio la kuwajengea uwezo wanawake wajasiriamali wa Wilaya ya Hanang mkoani Manyara kuhusu jinsi ya kuzibaini na kuzitumia fursa za kiuchumi, lililoandaliwa na Taasisi ya WEDAC Microfinance Institution Limited inayotoa mikopo na elimu ya fedha kwa wanawake wa vijijini.

Katika tukio hilo lililohudhuriwa na wanawake takribani 400, mtaalam wa ununuzi wa umma kutoka PPRA, Bi. Caroline Fungo aliwasilisha kuhusu fursa za zabuni za umma zilizotengwa na Serikali kwa ajili ya makundi maalum ambayo ni wa wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu. Bi. Fungo aliwahamasisha wanawake hao kuzingatia utaratibu wa kusajili vikundi vya watu watano hadi ishirini kwenye taasisi wezeshi kama Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, kisha kupata usaidizi wa kujisajili kwenye Mfumo wa NeSTi ili waombe zabuni zilizotengwa kwaajili yao.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya WEDAC, Bi. Joycelyn Umbulla amesema Taasisi hiyo imeshirikiana na PPRA kwakuwa wanawake wanapopatiwa mikopo yenye riba nafuu wanapaswa kufahamu kuwa kuna fursa za zabuni za umma, ambazo wanaweza kuwekeza katika kuzifanya ili waweze kurejesha mikopo, kupata faida na kukuza mitaji yao.

“WEDAC tunaamini kuwa mikopo ya riba nafuu tunayowapa wanawake wa vijijini ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuwainua wanawake ikiwa ni pamoja na hawa wa maeneo ya vijijini. Hivyo, tumewaalika PPRA tushirikiane katika kuwaonesha pia fursa za zabuni za umma ambazo Serikali yetu imezitoa kwa wananchi hadi ngazi za vijiji na mitaa, pamoja na upendeleo kwa makundi maalum,” amesema Bi. Umbulla.

“Lengo letu sote ni moja, kuhakikisha wanawake wanainuka kiuchumi. Ukimuinua mwanamke kiuchumi, tunaamini matokeo yake yatakuwa faida kwa kila mwana jamii. Tunawashukuru PPRA na Serikali kwa ujumla kwa jinsi inavyoshirikiana na wadau kuifikia jamii hadi ngazi za Kijiji,” ameongeza.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Mheshimiwa Rose Kamili Sukum aliwashukuru PPRA na WEDAC kwa kuweka mafunzo hayo kwa wakaazi wa Wilaya hiyo, ikieleza kuwa inaakisi kwa vitendo juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita kuwainua wanawake kiuchumi.

Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023 inazitaka taasisi zote nunuzi kutenga asilimia 30 ya bajeti ya ununuzi kwa ajili ya makundi maalum. Kwa mujibu wa PPRA, tangu Julai 1, 2023 hadi sasa, makundi maalum yamepata mikataba yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni Kumi na Tano.

No comments:

Post a Comment