DKT. HOMERA AZINDUA PROGRAMU YA ‘SEMA NA WAZIRI’ - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, March 17, 2026

DKT. HOMERA AZINDUA PROGRAMU YA ‘SEMA NA WAZIRI’


Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Juma Zuberi Homera, amezindua programu ya “Sema na Waziri” ikiwa ni hatua mpya ya kuimarisha mawasiliano kati ya Serikali na wananchi pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma za kisheria nchini.

Uzinduzi huo umefanyika leo Machi 17, 2026 jijini Dodoma, ambapo uliambatana na tukio la Waziri huyo kupokea simu za moja kwa moja kutoka kwa wananchi wa maeneo mbalimbali, akisikiliza changamoto zao na kutoa ufafanuzi wa masuala ya kisheria yanayowakabili.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Waziri Homera alisisitiza dhamira ya Serikali katika kusikiliza wananchi akisema:
“Samia Suluhu Hassan alitupa maelekezo kwamba tuhakikishe wananchi wanasikilizwa na kupata haki, na kusikiliza lazima tuwe na njia tofauti tofauti.”

Ameeleza kuwa, pamoja na Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, Wizara imeanzisha pia mfumo wa kituo cha simu (call center) kinachopokea na kushughulikia malalamiko ya wananchi ili kuwapatia ufumbuzi kwa wakati.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, programu ya “Sema na Waziri” ni mwendelezo wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi wanapata nafasi ya kueleza kero zao, hususan zinazohusu masuala ya sheria na haki.

Amefafanua kuwa, ingawa kituo cha huduma kwa wateja kilianzishwa Februari 14, 2024, uzinduzi wa programu hiyo unaongeza nguvu mpya katika utoaji wa huduma, ambapo sasa kutakuwa na mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Waziri na wananchi mara tatu kila mwezi.

Katika hatua nyingine, Waziri Homera amesema tangu kuanzishwa kwa kituo hicho, jumla ya malalamiko 2,023 yamepokelewa yakihusu masuala ya ardhi, ndoa, talaka, ajira, mirathi, ukatili wa kijinsia pamoja na matunzo ya watoto. Kati ya hayo, malalamiko 1,394 yameshapatiwa ufumbuzi huku 481 yakiendelea kufanyiwa kazi.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa programu hiyo kwa wananchi akieleza kuwa:
“Kuanzishwa kwa programu hii kunalenga kupunguza changamoto zilizokuwepo awali ambapo baadhi ya wananchi walilazimika kusafiri umbali mrefu kumfuata Waziri; sasa watapata huduma kwa njia ya simu.”

Katika moja ya simu zilizopokelewa, mwananchi kutoka Geita aliuliza kuhusu lini mchakato wa Katiba mpya utakamilika. Akijibu swali hilo, Waziri Homera alisema:

“Mchakato wa Katiba ni wa wananchi na ni sehemu ya Ilani ya CCM. Kwa sasa tunasubiri hatua zinazoendelea chini ya Rais, hivyo ni vyema kuwa na subira kwani jambo hili halijaachwa.”




No comments:

Post a Comment