RAIS STUBB AZINDUA MRADI WA EURO MILIONI 20 WA UHIFADHI WA MISITU – FORLAND - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, May 16, 2025

RAIS STUBB AZINDUA MRADI WA EURO MILIONI 20 WA UHIFADHI WA MISITU – FORLAND



Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam


Rais wa Jamhuri ya Finland, Mhe. Alexander Stubb, leo amezindua rasmi Mradi wa Kusimamia Uhifadhi wa Misitu, Matumizi Bora ya Ardhi na Kuongeza Thamani ya Mazao ya Misitu (Forestry, Land Use, and Value Chains Development in Tanzania – FORLAND), wenye thamani ya Euro milioni 20.

Mradi huo unalenga kukuza kanuni endelevu za uhifadhi wa misitu, kuboresha maisha ya wananchi, kuimarisha ukuaji wa uchumi wa Tanzania, pamoja na kuendeleza usimamizi wa misitu katika jamii, upandaji miti, na maendeleo ya mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu.

Katika hafla hiyo iliyofanyika Mei 16, 2025 katika Bustani ya Botanical Garden jijini Dar es Salaam, Rais Stubb ameshiriki katika zoezi la upandaji miti na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Tanzania na Finland katika sekta ya misitu.

“Nina imani mti nilioupanda utakua kama yalivyo mashirikiano kati ya nchi zetu katika sekta ya misitu, hususan kupitia mradi huu wa FORLAND,” amesema Rais Stubb.

Aidha, Rais Stubb ameeleza kuwa Finland ina misitu inayochukua asilimia 70 ya eneo la nchi hiyo, na kwamba bidhaa zake za misitu zinatambulika kwa ubora na uimara wake.

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb), amesema kuwa mradi wa FORLAND unatekelezwa katika mikoa ya Kusini mwa Tanzania, ukiwa na lengo la kuimarisha usimamizi wa rasilimali za misitu na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika jamii zinazozunguka misitu hiyo.

“Nchi yako (Finland) imekuwa mshirika muhimu kwa Tanzania katika sekta ya misitu, ikiwa imesaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali kama vile Mpango wa Usimamizi wa Eneo la Hifadhi ya Usambara Mashariki (1988–2002), vyuo vya misitu nchini Malawi, Tanzania na Zambia (1999–2005), Programu ya Kitaifa ya Misitu (2005–2010), pamoja na Biashara ya Kibinafsi ya Misitu na Kaboni (2010–2011),” amesema Mhe. Chana.

Ameongeza kuwa Finland pia imeisaidia Tanzania kupitia Programu za Kitaifa za Misitu na Nyuki (2013–2016), pamoja na Ufuatiliaji na Tathmini ya Rasilimali za Misitu (NAFORMA) tangu mwaka 2009.

Uzinduzi huo umehudhuriwa pia na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, pamoja na wanadiplomasia na viongozi waandamizi kutoka Serikali ya Tanzania na Finland.







No comments:

Post a Comment