SERIKALI INAENDELEA KUUNGANISHA MAKAO MAKUU YA MIKOA NA WILAYA KWA LAMI : WAZIRI MKUU MAJALIWA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, May 18, 2025

SERIKALI INAENDELEA KUUNGANISHA MAKAO MAKUU YA MIKOA NA WILAYA KWA LAMI : WAZIRI MKUU MAJALIWA


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali inaendelea kuhakikisha makao makuu ya mikoa na Wilaya zote nchini zinaunganishwa kwa barabara za lami ili kurahisisha huduma za usafiri na uchukuzi na hivyo kuchochea uchumi.

Mhe. Majaliwa ameeleza hayo leo Mei 18, 2025 wakati akizungumza na wananchi katika eneo la Hungumalwa Wilayani Kwimba Mkoani Mwanza na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji huo katika Mkoa wa Mwanza na kubainisha kuendelea kwa ujenzi wa barabara ya Hungumalwa - Ngudu hadi Magu kwa awamu ili ikamilike kwa kiwango cha lami.

“Niwahakikishie wananchi wa Kwimba lengo la Serikali ni kuzijenga barabara zinazounganisha makao makuu ya Mikoa na Wilaya ili ziimarike na tutaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mkakati huo kwani ni Maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan”, amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi Mhe. Abdallah Ulega ameeleza mkakati wa Wizara ya Ujenzi katika bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26 imepanga kujenga barabara ya Mobuki - Ngudu (km 26) kwa kiwango cha lami ambapo inaendelea na ujenzi wa Kilometa 10 kwa kiwango cha lami.

Ameongeza kuwa tayari Serikali imeanza ujenzi wa Kilometa tatu katika barabara ya Mobuki - Ngudu ili kuweza kuunganisha Wilaya ya Kwimba na Makao Makuu ya mkoa wa Mwanza.

Ametaja barabara nyingine ambazo zimepangwa kutekelezwa katika Wilaya hiyo ikiwemo ujenzi wa barabara ya Ngudu - Jojiro (km 10) unaendelea.

No comments:

Post a Comment