.jpg)
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, ametembelea banda la Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) katika maonesho ya mafanikio ya siku 100 za uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na utatuzi wa kero za wananchi.
Maonesho hayo ya siku tatu yamefunguliwa leo machi 5, katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma, yakishirikisha taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo TEMESA, ambapo imewasilisha mafanikio yao katika utoaji wa huduma kwa wananchi na kutoa elimu kuhusu majukumu yao.
Akiwa katika banda la TEMESA, Mhe. Senyamule alipata maelezo kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na TEMESA pamoja na mafanikio ya Wakala kutoka kwa Meneja Masoko na Uhusiano kwa Umma, Bi. Martha Joachim.

Akitoa ufafanuzi huo, Bi. Martha amesema TEMESA imepiga hatua katika kuboresha utoaji wa huduma za kiufundi kwa taasisi za Serikali kupitia matumizi ya mifumo ya kisasa na ya kidijitali.
Ameeleza kuwa miongoni mwa mafanikio hayo ni matumizi ya Mfumo wa Usimamizi wa Kazi za Matengenezo (MUM), unaosaidia na kurahisisha ufuatiliaji wa shughuli za matengenezo kwa ufanisi zaidi.

“Mfumo huu umeongeza uwazi, ufanisi na kasi katika utoaji wa huduma za matengenezo, na kusaidia taasisi za Serikali kupata huduma bora zinazopelekea kuwahudumia wananchi kwa ufanisi,” amesema.
Aidha, Bi. Martha ameongeza kuwa TEMESA inaendelea kuboresha utendaji kazi wake, hasa katika huduma za matengenezo ya magari ya Serikali, usimamizi wa vivuko pamoja na miundombinu ya umeme katika taasisi mbalimbali za Umma.

No comments:
Post a Comment