PROF. SHEMDOE AIPONGEZA MANISPAA YA TEMEKE KWA MPANGO MKAKATI WA MIAKA 10 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, March 5, 2026

PROF. SHEMDOE AIPONGEZA MANISPAA YA TEMEKE KWA MPANGO MKAKATI WA MIAKA 10


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa - TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kwa kuandaa Mpango Mkakati wa Maendeleo wa miaka kumi ijayo, akisema ni hatua muhimu ya kupanga mustakabali wa wananchi kwa mtazamo wa muda mrefu.

Prof. Shemdoe ametoa pongezi hizo leo Machi 4, 2026, katika kikao kazi cha pamoja na timu ya uongozi wa Halmashauri hiyo cha kuwasilisha mpango mkakati huo, kilichofanyika katika Ofisi Ndogo ya Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI Magogoni, Jijini Dar es Salaam.


“Niwapongeze sana kwa kuandaa mpango huu wa miaka kumi. Hii ni Halmashauri ya kwanza kufikiria nini kitatokea miaka kumi ijayo, naomba halmashauri nyingine pia ziige mfano huu wa kufikiria kuhusu siku zijazo,” amesema Prof. Shemdoe.

Aidha, ameitaka Halmashauri hiyo kuhakikisha mpango mkakati huo unaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Mwaka wa Taifa ili kuleta tija na matokeo chanya kwa wananchi.

Katika hatua nyingine, Prof. Shemdoe amepongeza mshikamano na ushirikiano uliopo ndani ya wilaya ya Temeke, akieleza kuwa ajenda za pamoja za maendeleo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha viongozi na watendaji wanafanya kazi kwa umoja kwa manufaa ya Watanzania.

Awali akiwasilisha mpango huo, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Sixtus Mapunda, amesema mpango huo umejikita katika vipaumbele muhimu ikiwemo elimu, afya, miundombinu ya barabara, biashara, kupunguza foleni pamoja na maendeleo ya sanaa na michezo, kwa lengo la kuendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi wa Manispaa ya Temeke.

No comments:

Post a Comment