
Tarehe 1 Februari 2025 Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua rasmi Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023 inayolenga kutoa elimu inayozingatia ujuzi kulingana na mahitaji ya soko la ajira na kuchangia katika maendeleo ya Taifa.
Serikali imeendelea kutoa mafunzo kwa walimu ikiwemo utekelezaji wa mitaala iliyoboreshwa kwa walimu 70,657 (shule za msingi 3,403 na sekondari 67,254) ikilinganishwa na walimu 1,250 wa shule za msingi na sekondari waliopata mafunzo mwaka 2021/22. Aidha, imetoa mafunzo kwa wathibiti ubora wa shule 611 ikilinganishwa na wathibiti ubora wa shule 368 waliopata mafunzo mwaka 2021/22. Vilevile, Serikali imetoa mafunzo kwa maafisa elimu kata 403, wakufunzi wa vyuo vya ualimu 70, watumishi wa vyuo vya ualimu 120, wakuu wa vyuo 35 na walimu wakuu 9,020.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda (Mb) ameyasema hayo bungeni Jijini Dodoma leo tarehe 12 Mei 2025 wakati akiwasilisha Makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo na kusema kuwa katika kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa sera na mitaala iliyoboreshwa, Serikali imeanza mapitio ya Sheria ya Elimu Sura ya 353 ili kuendana na matakwa ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023 ambapo maoni ya wadau mbalimbali wa elimu kuhusu sheria husika yameendelea kukusanywa.
Waziri Mkenda ameeleza kuwa serikali imeandaa rasimu ya marekebisho ya Sheria ya VETA, Sheria ya Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na Sheria ya Mfuko wa Elimu (TEA). Aidha, Serikali imekamilisha taarifa ya mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Bodi ya Huduma za Maktaba pamoja na mapendekezo ya marekebisho ya kifungu cha 58 cha Sheria ya Vyuo Vikuu, Sura ya 346 na kanuni ya 33 ya Kanuni za Vyuo Vikuu. Vilevile, imefanya marekebisho ya Sheria Ndogo za Chuo Kikuu cha Dodoma kwa ajili ya kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali. Marekebisho ya sheria hizo yanalenga kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa sera na kuwezesha taasisi hizo kuendana na makubaliano ya kikanda na kimataifa.
Vilevile, Serikali imeandaa Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Teknolojia za Kidijitali katika Elimu wa Mwaka 2024/25-2029/30 sambamba na miongozo minne (4) kwa ajili ya utekelezaji wa Mkakati huo kama ifuatavyo: Mwongozo wa Ujumuishi wa Matumizi ya Teknolojia za Kidijitali katika Shule na Vyuo vya Ualimu 2025; Mwongozo wa Matumizi ya Teknolojia za Kidijitali katika Vyuo vya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi 2025; Mwongozo wa Matumizi ya Teknolojia za Kidijitali katika Vyuo Vikuu 2025; na Mwongozo wa Matumizi ya Akili Unde (Artificial Intelligence) katika Elimu 2025;
Waziri Mkenda amesema kuwa serikali imetoa Mwongozo wa Matumizi ya Breli wa Mwaka 2025 ili kuimarisha matumizi ya breli katika nyanja mbalimbali. Vilevile, imetoa Mwongozo wa Kitaifa wa Elimu Jumuishi wa Mwaka 2025 kwa lengo la kuhakikisha mfumo wa elimu unawajumuisha wanafunzi wote kwa kutoa fursa za ujifunzaji zinazokidhi mahitaji.



No comments:
Post a Comment