Na John Mapepele
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe.Mohamed Mchengerwa amezindua soko la kisasa la nyama choma la Kumbilamoto vingunguti, Ilala jijini Dar es Salaam na kushuhudia utiaji wa mikataba ya miradi 6 ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 7.7
Mara baada ya kuzindua soko hilo ambalo limegharimu takribani shilingi milioni 727 amepongeza uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kufanikisha mradi huo ambapo amezitaka Halmashauri nyingine kuiga mfano huo.
Aidha, amefafanua kuwa soko hilo litakwenda kuwapatia ajira wananchi wengi huku akisisitiza kuendelea kulitunza ili lisiharibike kwenye kipindi kifupi.
Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa kukamilika kwa soko hilo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na kufafanua kuwa Serikali ya awamu ya sita tayari imekamilisha miradi mingi kama iilivyoahidi.
Wakati huo huo Waziri Mchengerwa amezitaka Halmashauri zote nchini kutimiza malengo zilizojiwekea ya ukusanyaji mapato ili ziweze kutekeleza miradi ya maendeleo huku akizitaka kuendelea kubuni miradi mbalimbali ya maendeleo yenye tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
Akizungumzia kuhusu wakandarasi wazawa, Mhe Mchengerwa amezitaka Halmashauri na mikoa yote nchini kuwapa kipaumbele wakandarasi wazawa huku akitoa wito kuwachukulia hatua wakandarasi wanaofanya vibaya katika kazi wanazopewa.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogole amemhakikishia Mhe. Mchengerwa kuwa mikataba yote iliyosainiwa inakwenda kukamilika kabla ya mwisho wa mwaka na kwamba wananchi watakwenda kunufaika na miradi hiyo.
Katika uzinduzi wa soko hilo Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Zungu ambaye pia ni Mbunge wa Ilala amewataka watanzania kutojihusisha na uvunjaji wa amani katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu
Bi. Amina Selemani ambaye ni miongoni mwa mfanyabiashara katika soko hilo amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kutoa fedha za kujenga soko hilo ambalo limetoa ajira kwa akina mama wengi.
“Kwa kweli tunamshukuru Mheshimiwa Rais wetu kwa upendo huu wa kutuletea mradi huu wa soko ambao umekuwa ni ukombozi kwa maisha yetu”. Amefafanua Amina
No comments:
Post a Comment