WANANCHI KUUNGANISHWA NA KADI ZAO ZA NIDA KUPITIA KADI MOJA JAMII - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, May 15, 2025

WANANCHI KUUNGANISHWA NA KADI ZAO ZA NIDA KUPITIA KADI MOJA JAMII



Serikali inaendelea na mchakato wa kuwaunganisha wananchi na huduma mbalimbali kupitia kadi moja ya Jamii ambayo itahusishwa na taarifa zao za NIDA.

Kadi hiyo itawawezesha wananchi kufanya miamala ya kifedha na kupata huduma mbalimbali kwa kutumia kitambulisho kimoja.

Kadi hiyo ya Jamii itatumika katika maeneo mbalimbali ikiwemo viingilio vya viwanja vya mpira, malipo ya vivuko, usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka (UDART), taasisi za kifedha na malipo mengine muhimu ya huduma kwa umma.

Akizungumza baada ya ziara ya Mhe. Kassim Majaliwa(Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alipotembelea Kituo cha Kuhifadhi Data Kimtandao (NIDC) kwa lengo la kuangalia Mfum wa N- CARD unavyofanya kazi,Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Slaa, alisema Serikali imejipanga kuhakikisha mifumo yote inasomana kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi kupitia Mradi wa Digital Tanzania.

Amesema serikali itahakikisha taasisi zote nchini zinahifadhi data zao NIDC kwa gharama nafuu na kwa usalama wa uhakika, huku akibainisha kuwa Mradi wa Digital Tanzania, ambao ni sehemu ya utekelezaji wa Kadi Jamii, unaendelea kutekelezwa kwa lengo la kuunganisha huduma zote kwa njia ya kidijitali.

"Mradi huu utarahisisha utoaji wa huduma mbalimbali za kidigitali, ikiwemo mihamala ya kifedha, kwa kuhakikisha kuwa mifumo yote inasomana. Wananchi hawatalazimika tena kubeba kadi nyingi bali watatumia kadi moja tu ya jamii," alisema Waziri Slaa.



Ameeleza kuwa katika bajeti ya mwaka 2024/2025, serikali ilitenga Shilingi bilioni 10 kuiwezesha NIDC kutekeleza mradi huo wa Digital Tanzania. Kupitia mradi huo, taasisi za umma na binafsi hazitahitaji kuwekeza katika mifumo yao binafsi bali zitatumia huduma ya pamoja kupitia NIDC kwa gharama nafuu.

Aidha, Waziri Slaa amesema kuwa serikali ina mpango wa kuhakikisha kila mwananchi anamiliki simu janja kwa kupunguza gharama ya simu hizo ili ziweze kutumika pamoja na Kadi Jamii hiyo.

Kuhusu mawasiliano, Waziri amesema kuwa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano unaosimamiwa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) tayari umeunganisha wilaya 109, huku wilaya 30 zikiwa zinakamilishiwa, na baadhi ya nchi jirani za Afrika tayari zimeunganishwa na mkongo huo.

No comments:

Post a Comment