WANANCHI RUFIJI WAMPONGEZA MCHENGERWA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, May 10, 2025

WANANCHI RUFIJI WAMPONGEZA MCHENGERWA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO



Na. James K. Mwanamyoto OR-TAMISEMI


WANANCHI wa Rufiji mikoani Pwani wameeleza kufurahishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo jimboni humo ikiwemo ujenzi wa barabara, shule, zahanati na vituo vya afya.

WANANCHI hao pia wamempongeza Mbunge wa Rufiji, Mhe. Mohamed Mchengerwa kwa jitihada zake za kuhakikisha huduma za jamii zinapatikana kwa uhakika na ubora.

Wameyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati wa ziara ya kikazi ya Mwenyekiti wa UWT taifa Mhe. Mary Chatanda aliyoifanya Wilayani Rufiji kwa siku mbili, kwa lengo la kukagua utetelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2020/2025.

Mkazi wa ikwiriri Bw. Abdallah Moba amesema jitihada za Mhe. Mchengerwa za kujenga barabara ya Kituo cha Afya Ikwiriri zimewawezesha wananchi kufika kwa urahisi katika kituo hicho ili kupata huduma za afya msingi.

Bi. Mariam Hamza ambaye ni Mama Lishe amesema kuwa, kabla ya barabara ya Kituo cha Afya Ikwiriri kujengwa wateja wake walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya vumbi pindi bodaboda zinapopita, hali iliyopelekea kuwapoteza wateja lakini hivisasa changamoto hiyo imetatuliwa.

Bw. Sirajidini Hassan ambaye pia ni dereva bodaboda ambaye shughuli zake anazifanya nje ya Kituo cha Afya Ikwiriri, amemshukuru Waziri Mchengerwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuijenga barabara hiyo ya Kituo cha Afya Ikwiriri na kuiwekea taa kwani hapo awali watu hususani wanawake walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya kuporwa mali zao kutokana na kiza kilichokuwepo wakati usiku.

Bw. Ramadhan Hamza ambaye pia ni dereva bodaboda, amemshukuru Waziri Mchengerwa kwa kuhakikisha Barabara ya Kituo cha Afya Ikwiriri inajengwa, na hatimaye kuwawezesha wagonjwa kufika kwenye kituo hicho cha afya kwa wakati ikiwa ni pamoja na kuwawezesha madereva bodaboda kujiongezea kipato.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema amefanya kazi usiku na mchana ya kuleta mabadiliko wilayani Rufiji kwa kushirikiana na viongozi wa kata zote, lengo likiwa ni kuboresha upatikianaji wa huduma za kijamii ambapo wananchi hivisasa wanafurahia huduma zinazotolewa katika sekta ya elimu, afya na barabara.
Mhe. Mchengerwa amesema:


“Tumefanya kazi usiku na mchana kuhakikisha tunaibadilisha Rufiji, tulianza ujenzi wa shule, ujenzi wa zahanati, ujenzi wa vituo vya afya na miundombinu ya barabara na mingineyo,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.


Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa, walikubaliana kwamba ndoto ya wanarufiji ni kuleta mabadiliko, hivyo ana uhakika mwananchi yeyote akiulizwa hivisasa ataeleza namna ndoto hiyo ilivyotimia katika kipindi hiki cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita.


Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Ikwiriri Dkt. Tegemei Mtambo ameishukuru Serikali kwa kuwapatia milioni 140 zilizowezesha ujenzi wa jengo la huduma za mionzi na huduma tayari imeanza kutolewa, ambapo awali wananchi walilazimika kusafiri zaidi ya kilomita 30 kufuata huduma hiyo katika Hospitali ya Wilaya na Hospitali ya Misheni Mchukwi.


Sanjari na hilo, Dkt. Mtambo ameishukuru Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa kuwapatia X-Ray ya kisasa inayowahudumia wananchi, aidha amemshukuru Waziri Mchengerwa kwa kutimiza ahadi yake ya kumleta Mteknolojia wa Mionzi ikiwa ni pamoja usimamizi wa maboresho yote yaliyofanyika kiasi cha watu kuamini kuwa Kituo cha Afya Ikwiriri ndio Hospitali ya Wilaya ya Rufiji.






No comments:

Post a Comment