WANANCHI WA KATA YA CHANG’OMBE DODOMA WAPONGEZA MIKAKATI YA JESHI LA POLISI KUPITIA MICHEZO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, May 24, 2025

WANANCHI WA KATA YA CHANG’OMBE DODOMA WAPONGEZA MIKAKATI YA JESHI LA POLISI KUPITIA MICHEZO



Wananchi wa Kata ya Chang’ombe, Jijini Dodoma, wamepongeza mkakati wa Jeshi la Polisi wa kuwafikia vijana kupitia michezo, jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa matukio ya uhalifu katika eneo hilo na kuongeza ushiriki wa wananchi katika vikundi vya ulinzi shirikishi.

Haya yamejiri Mei 24, 2025, katika sherehe ya kusherehekea ushindi wa ubingwa wa Ligi ya Mpira wa Miguu iliyoandaliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma chini ya Kamanda wa Polisi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Katabazi, kupitia mashindano ya Umoja Polisi Jamii Cup. Mashindano hayo yalihitimishwa hivi karibuni kwa timu ya Chang’ombe Chama la Wana kutwaa ubingwa kwa kuifunga timu ya Mpunguzi FC, ambapo zawadi ya kombe, ng’ombe na mbuzi zilitolewa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kamanda Katabazi aliipongeza timu ya Chang’ombe pamoja na wananchi kwa kuonesha kiwango bora cha soka miongoni mwa zaidi ya kata 14 zilizoshiriki mashindano hayo.

Aidha, Kamanda Katabazi aliwasisitiza wananchi kuendelea kuchukia uhalifu na kutoa taarifa kwa wakati kuhusu vitendo vya kihalifu ili hatua stahiki zichukuliwe mapema kabla madhara hayajatokea.

“Chang’ombe mmekuwa mfano wa kuigwa katika Jiji la Dodoma. Mmefanya vizuri kwenye michezo na mmekuwa na mabadiliko makubwa. Zamani eneo hili lilisifika kwa matukio ya uhalifu, lakini sasa hali ni tofauti kabisa. Endeleeni kuchukia uhalifu na msijihusishe kwa namna yoyote,” alisema Katabazi.

Vilevile, aliwaasa wazazi na walezi kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika malezi ya watoto wao, na kushirikiana na Polisi Kata pindi wanapokumbana na changamoto za kiusalama, pamoja na kushiriki katika shughuli za maendeleo ya jamii.

Kwa upande wake, mlezi wa timu ya Chang’ombe, ambaye pia ni Polisi Kata wa eneo hilo, Samweli Gwivaha, alieleza kuwa michezo imekuwa nyenzo muhimu ya kuimarisha ushirikiano kati ya Polisi na wananchi katika kuzuia na kutatua uhalifu.

Wananchi wa Kata ya Chang’ombe walieleza kufurahishwa na juhudi za Jeshi la Polisi kupitia Kamanda wa Mkoa, kwa kutumia michezo kama jukwaa la kuwaunganisha vijana na kuwaelimisha juu ya masuala ya ulinzi na usalama. Walisema kuwa kwa sasa hali ya amani imetamalaki na uhalifu umepungua kwa kiwango kikubwa.

Mashindano hayo yalilenga kuwakutanisha vijana wa maeneo mbalimbali, kuwapa elimu ya ulinzi na kuhamasisha ushiriki wao katika vikundi vya ulinzi shirikishi ili kujenga jamii salama na yenye mshikamano.







No comments:

Post a Comment