Wabunge Wanawake wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamenufaika na elimu ya akili mnemba yatakayowawezesha kutumia teknolojia mpya katika kuharakisha upatikanaji wa maendeleo.
Akizungumza katika Semina iliyofanyika Jijini Dodoma Mwakilishi wa Afrika, wa Women Political Leaders (WPL) Mb. Neema Lugangira amesema fursa hiyo ya mafunzo juu ya matumizi ya akili mnemba (AI) ambayo ni sehemu ya mradi Barani Afrika unaojulikana kama Female AI Leaders (FemAI) unalenga kuchagiza na kuimarisha uwezo na uelewa wa viongozi wanawake katika siasa na maendeleo yao kwa ujumla kwa kutumia teknolojia kama akili mnemba.
Aidha, ameongeza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kufahamu vyema mifumo ya nchi kisera na kisheria kwa kutumia teknolojia mpya kama akili mnemba.
"Ni muhimu sana kwetu viongozi na wabunge tujue namna ya kutumia teknolojia mpya ya akili mnemba maana hatua hii itatusaidia kurahisisha kazi zetu na kutekeleza majukumu yetu" amesema Mbunge Lugangira.
Vilevile amebainisha kuwepo kwa fursa mbalimbali zinazotokana na matumizi ya akili mnemba katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, afya, na nyinginezo sambamba na changamoto za matumizi ya AI pale yasipotumika kwa umakini kama kusababisha ukatili wa kijinsia, kurubuni watoto na kufifisha uwezo wa kufikiri na kuwa tegemezi.
"Katika kipindi hiki tunapoelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu Oktoba 25, sisi kama wabunge itatusaidia kuandaa mikakati ya kampeni katika maeneo yetu na uzuri tulifanya jaribio na tukajiinea AI inavyofanya kazi" ameeleza Mb.Lugangira.
Hata hivyo ameshukuru kufanikisha semina hiyo kupitia Shirika lake la OMUKA Hub kwa ushirikiano mkubwa wa Bunge la Tanzania.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kaamti ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mhe Fatma Toufiq akimwakilisha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt Tulia Ackson Mwansansu, amesema matumizi ya Akili mnemba (AI) ni ya muhimu kwenye kwenye sekta mbalimbali ikiwemo elimu, kilimo, mazingira na Bunge inayachukulia kwa uzito na wanajipanga kuandaa sera na sheria za usimamizi.
"Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limefurahi kuwa sehemu ya kunufaika na mafunzo haya ya teknolojia ya Akili mnemba" amesema Mb. Fatma.
Katika namna hiyo hiyo Mbunge wa Iringa mjini Jesca Msambatavangu aliyeshiriki semina hiyo amesema ni muhimu kukubaliana na mabadiliko ya teknolojia ili kwenda Dunia inavyotaka.
"Tulikuwa tukitumia akili bandia bila kujua, mfano matumizi ya (Google) na kutupatia taarifa, unaweza kuona kwamba si kitu kigeni kwani tumeelezwa kuwa matumizi ya akili bandia yameanza zamani sana mnamo mwaka 1950, kwetu hii ni fulsa kubwa na mimi kama Mbunge nitaweza kuwafundisha wanawake wenzangu faida na namna ya kukabiliana na changamoto za Matumizi ya akili bandia" amefafanua Mbunge Msambatavangu
No comments:
Post a Comment