
Na Jeremia Mwakyoma
DODOMA
Watalaamu mabingwa wa wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) leo wamepigwa msasa kwa kupatiwa mafunzo ya maadili katika semina ya siku moja iliyofanyika katika ukumbi wa Tume ya Taifa ya Takwimu jijini Dodoma.
Akitoa hotuba yake katika mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa BMH na Mkurugenzi wa Upasuaji Dkt. Henry Humba amesema kuwa mafunzo hayo ni endelevu na yatatolewa kwa awamu kwa madaktari wa Vitengo vingine pia na kusisitiza malengo yake ni kuboresha utumishi wa umma unaozingatia maadili.
"Malengo ya mafunzo hayo ya maadili kwa Madaktari Bingwa wa Upasuaji ni kuendelea kuwashirikisha maono ya Serikali ya kuhakikisha kuna kuwa na huduma bora kwa Wananchi kutoka kwa Watendaji na Wataalamu wa Serikali ambazo zimezingatia maadili ya Utumishi wa Umma" alisisitiza Dkt. Humba.
Dkt. Humba alitumia fursa ya mafunzo hayo.kuwajulisha Madaktari Bingwa wa Upasuaji (na Idara nyingine) kutambua kuwa uelekeo wa Hospitali ya Benjamin Mkapa kuwa Hospitali ya Rufaa ya Taifa na hivyo inatakiwa kuwa na utamaduni unaokubalika na unaoendana na hadhi hiyo kubwa ikiwemo miiko ya kazi na maadili huku akiwatangazia Madaktari Bingwa wa Upasuaji juu ya Hatua za Uongozi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa kuanzisha Kamati ya Usimamizi wa Vyumba vya Upasuaji (Theatre Committee).
"Lengo la kamati hii ya Usimamizi wa Vyumba vya Upasuaji katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (Theatre Committee) ni kuboresha na kuongeza kiwango cha utendaji wa mtumishi mmoja mmoja, ufanisi wa theatre zetu na Taasisi kwa ujumla, aidha kufanya ufuatiliaji na tathimin ya utekelezaji wa watumishi katika huduma za upasuaji na wote tunaohusika tushiriki ipasavyo" alisisitiza Dkt. Humba.
Nae Ndg. Salvatory Kaiza Mwezeshaji wa mada ya Maadili ya Utumishi wa Umma aligusia kuhusu taratibu, misingi na maadili ya utumishi wa Umma na kuwataka Madaktari hao kuvifuata kutokufanya hivyo kunaweza kuwasababisha kuchukuliwa hatua za kinidhamu na za kisheria.
"Kwa Mtumishi wa Umma kutotimiza Wajibu uliopangiwa na kutotimiza kwa ufasaha ni kukiuka maadili ya Utumishi wa Umma, Madaktari wote ni lazima msimamie na kutekeleza Miongozo ya Madaktari na Viapo vya Madaktari mnavyoapa na kuzingatia maadili ya ujumla ya utumishi wa Umma, kutofanya hivyo unaweza kuchukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria" alikazia Ndg. Kaiza.
Aliongeza kuwa Hospitali ya Benjamin Mkapa iko katika mchakato wa kuwa Hospitali ya Rufaa ya Taifa, na kwa huduma zake wananchi wanatoka hadi mikoa mbalimbali hata yenye Hospitali kubwakubwa kama Dar es salaam kuja BMH kufuata huduma zake, lazima Madaktari na Watumishi wote kutoa huduma bora na kuzingatia maadili ili kulinda imani hiyo ya Wananchi walionayo juu ya BMH.
"Tabia za kukosa heshima, uadilifu, uaminifu, kutozingatia maadili, kauli mbaya, ulevi, upendeleo, kutotunza na kujinufaisha binafsi kwa vifaa tiba na madawa ya taasisi, kuhudumia wagonjwa wachache chini ya uwezo, kupokea malipo mara mbilimbili, vitendo vya Rushwa, kuchochea migogoro kati ya Wananchi na Serikali kwa kutokutoa huduma au kutoa huduma zenye kasoro, kutotunza siri za kazi na za wagonjwa ni kukiuka maadili ya utumishi wa Umma, kuna athiri utendaji binafsi wa Madaktari na taasisi kwa ujumla" alimalizia Ndg. Kaiza
Bi. Suzana Raymond Mwezeshaji kutoka TAKUKURU aliwataka Madaktari kuwachukulia Wagonjwa wanaokuja kupata matibabu Hospitali ya Benjamin Mkapa kama vile Mama zao, Baba zao, Wadogo zao, Kaka zao, Watoto wao na ndugu zao waliowaacha nyumbani ili wawahudumie kwa upendo jambo ambalo litaepusha malalamiko mengi likiwemo lalamiko la Rushwa.
" Ni muhimu kwa Madaktari kuhakikisha vipato mnavyovipata viwe kwa njia za halali na mtambue kuwa ni kosa kisheria kwa Mtumishi kutumia mali aliyopewa aisimamie na kuitumia kwa matumizi ya Serikali kuwahudumia Wananchi kuitumia mali hiyo kujinufaisha binafsi, na tusisitize matumizi ya Teknolojia ni muhimu katika kupunguza au kuondoa Mazingira yanayoweza kuchangia Rushwa" alibainisha Bi Suzana.
Prof. Masumbuko Mwashambwa kutoka Chuo Kikuu Dodoma na Mwezeshaji wa Maadili ya Upasuaji na Mentorship alisisitiza umuhimu wa Madaktari wa Upasuaji kujipanga vizuri katika maamuzi yao na matibabu ya upasuaji wanayotoa ili kuhakikisha usalama wa Mgonjwa kwa kuzingatia baadhi ya operesheni wanazozifanya ni za kipekee na nyingine zinahitaji uangalifu mkubwa ili mgonjwa asipoteze maisha au asipate madhara baada ya kufanyiwa opereshen na kuwalea madaktari wachanga.
"Kuwafanyia mentorship Madaktari wachanga au walio masomoni ni jambo la muhimu sana kwakuwa inasaidia kuzalisha Madaktari bora wenye uwezo mkubwa ambao wataendeleza sekta ya Afya kutibu Wananchi alifafanua Prof. Mwashambwa.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu wa BMH Ndg. Theophory Mbilinyi alihitimisha mafunzo hayo kwa kuwakumbusha Madaktari Bingwa wa Upasuaji kuwa Utumishi wa Umma unaendeshwa kwa Sheria, Taratibu na Kanuni; kuna Viongozi, kuna Ilani ya Chama Tawala na Vipaumbele vya kuboresha huduma kama ambavyo Viongozi wanavyowaahidi Wananchi na kuwataka madaktari kutambua kuwa Viongozi hawafanyi kazi hizo peke yao, Wanateua Wakuu wa Taasisi na Serikali inaweka Watumishi kwa ajili ya kutekeleza majukumu hivyo lazima kuzingatia maelekezo, maagizo na kuwa na nidhamu ya kazi"
Miongoni mwa mada zilizofundishwa katika Kikao hicho ni pamoja na Maadili ya Utumishi wa Umma, Elimu ya kuhusu Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Wajibu wa Watumishi katika kuzuia na kuoambana na Rushwa), Uadilifu Binafsi na wa Taasisi (Kuweka Siri), Maadili ya Upasuaji na Mentorship na Uzingatiaji wa Maadili ya Kitaaluma kwa Madaktari wa Tiba, Meno na Wataalamu Wasaidizi wa Afya.










No comments:
Post a Comment