Rais mpya wa Baraza la 14 la Usimamizi wa Mkataba wa Lusaka (LATF), Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, ametoa wito kwa nchi wanachama wa Mkataba huo kushirikiana katika uwekezaji wa teknolojia, uvumbuzi, na mifumo ya kisasa ya utawala ili kuimarisha maendeleo katika sekta mbalimbali za uhifadhi wa maliasili.
Akizungumza wakati wa kukabidhiwa rasmi nafasi ya urais wa Baraza hilo katika Mkutano wa 14 wa LATF unaofanyika leo Mei 8, 2025, jijini Arusha, Mhe. Chana ambaye ni Waziri wa Maliasili na Utalii, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda katika kulinda na kuhifadhi bioanuai ya mimea na wanyama.
“Kwa niaba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nawakaribisha jijini Arusha – Mji wa kidiplomasia wa Afrika Mashariki, mahali ambapo amani, umoja na maendeleo hukutana. Mkutano huu si wa kikanuni tu, bali ni ishara ya mshikamano wetu wa Afrika katika kukabiliana na vitisho vya kimataifa kwa mazingira yetu, uchumi na uhuru wa mataifa yetu,” amesema Mhe. Chana.
Amebainisha kuwa Mkataba wa Lusaka umeendelea kuwa alama ya mshikamano na juhudi za pamoja za kupambana na uhalifu dhidi ya wanyamapori. Aidha, alisema mkataba huo si chombo tu cha kisheria, bali ni jukwaa linalowezesha ushirikiano wa kikanda, kubadilishana taarifa, uzoefu, na kutafuta suluhisho za pamoja za changamoto zinazowakabili wanachama.
Akizungumzia mafanikio ya Tanzania, Mhe. Chana ameeleza kuwa katika muongo uliopita, taifa limepiga hatua kubwa katika kupambana na uhalifu wa wanyamapori na kuimarisha juhudi za uhifadhi. Alitaja miongoni mwa hatua zilizochukuliwa kuwa ni pamoja na maboresho ya sheria, ikiwemo marekebisho ya Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori.
Pia, amesema kuanzishwa kwa Huduma ya Uhifadhi wa Wanyamapori na Misitu (WFCS); Ushirikiano wa kimataifa na kikanda ulioboreshwa;Uhamasishaji wa jamii kuhusu umuhimu wa uhifadhi;
Uvumbuzi wa kiteknolojia kwa ajili ya ufuatiliaji na udhibiti wa uhalifu wa wanyamapori;Hatua kali dhidi ya mitandao ya usafirishaji haramu wa wanyama.
“Juhudi hizi zimeungwa mkono na kutambuliwa na jamii ya kimataifa, na sasa ni wakati mwafaka kwa nchi wanachama wa LATF kuanza kutekeleza Mpango Mkakati wa LATF 2025–2030, ambao ni nyenzo muhimu katika kufikia malengo yetu ya pamoja,” ameongeza.
Kadhalika, Mhe. Chana amehitimisha hotuba yake kwa kutoa pongezi za dhati kwa Mhe. Rebecca Miano, Waziri wa Utalii na Wanyamapori wa Jamhuri ya Kenya, kwa uongozi wake bora katika kipindi cha miaka miwili iliyopita akiwa Rais wa Baraza hilo.
No comments:
Post a Comment