DKT JINGU AWATAKA VIJANA KUCHANGAMKIA FURSA ZA KIUCHUMI NA KULINDA AMANI YA NCHI. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, June 21, 2025

DKT JINGU AWATAKA VIJANA KUCHANGAMKIA FURSA ZA KIUCHUMI NA KULINDA AMANI YA NCHI.



Na WMJJWM- Dar Es Salaam




Katibu Mkuu wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu amewataka vijana kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazotolewa na Serikali ili kujiajiri na kuajiri wengine na kudumisha umoja, utulivu na amani kwa maendeleo ya Taifa.


Dkt Jingu ameyabainisha hayo Juni 21, 2025 mkoani Dar Es Salaam wakati akizungumza kwenye Tamasha la Vijana la Twenzetu kwa Yesu lililoandaliwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).


Dkt. Jingu amesema Serikali imefungua mifuko katika nyanja mbalimbali kuwawezesha vijana nchini (Tanzania Bara) kupata mitaji kwa njia ya mikopo yenye masharti nafuu ili kuanzisha au kuendeleza miradi yao ya uzalishaji mali. Kupitia mikopo hiyo, vijana wanajitegemea, wanapunguza umaskini wa kipato na kujiajiri wenyewe.


"Vijana wa Tanzania ni nguvu kazi kubwa yenye maarifa, uwezo na ubunifu, Makadirio ya idadi ya Watu ya mwaka 2025 kwa Tanzania Bara yanaonesha kuwa idadi ya vijana wenye umri kati ya 15 - 45 ni asilimia 42.7 ya jumla ya idadi ya watu wote nchini, Takwimu hizi zinaonesha kuwa Tanzania ina nguvu kazi kubwa ya vijana ukiondoa watoto, hivyo vijana tutumie fursa zilizopo kujikwamua kiuchumi" amesema Dkt. Jingu


Amesema kukua kwa Teknolojia na ubunifu (digital innovation)
ni mojawapo ya maeneo yenye nafasi za kiuchumi kwa vijana hasa katika masuala ya ubunifu wa kiteknolojia (app ya mifumo ya biashara mtandaoni), ubunifu wa mavazi, sanaa, na filamu, ufundi wa kiufundi na utengenezaji wa bidhaa (crafts, vifaa vya majumbani),hivyo ni muhimu kujifunza na kuanzisha shughuli hizo na kujiongezea kipato.


"Kila sekta nchini ina fursa za kuwezesha vijana kujiajiri. Hivyo, kinachotakiwa ni vijana kuzifikia sekta na kutumia mitandao kujiendeleza katika kupata ujuzi utakaowawezesha kutumia fursa zilizopo kwenye sekta hizo" amesisitiza Dkt. Jingu.

Amezitaja baadhi ya fursa hizo kuwa ni pamoja na mikopo kwa vijana ya asilimia kumi inayotolewa katika halmshauri zote nchini, Mikopo kwa wafanyabiashara ndogondogo inayotolewa na Benki ya NMB ambapo mikopo hiyo inaratibiwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum.

Pia ametoa wito kwa vijana kutimiza wajibu wao katika kudumisha amani, ulinzi, heshima, utii na nidhamu kwa viongozi wa wa nchi ili kudumisha umoja, utulivu na maendeleo ya nchi.

"Maadili, heshima, nidhamu na uzalendo ni msingi wa mwenendo mwema wa kijana kwa Taifa lake. Utii kwa Mamlaka siyo udhaifu bali ni njia ya kuonesha uzalendo, utu na uaminifu kwa Taifa letu. Kijana anayemheshimu Rais wake, viongozi wa Serikali, walimu na wazazi wake ujenga msingi bora wa maisha yake na uongozi wa kesho kwa Taifa letu.“ amefafanua Dkt. Jingu

Aidha amewaomba vijana kumpenda na kumtumikia Mungu kwa moyo safi, kuwa watenda mema, kuilinda amani, ushirikiano na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kujenga Taifa, ikiwa ni pamoja na kutimiza wajibu wao wa kikatiba wa kugombea na kuchagua Viongozi katika uchaguzi mkuu ujao.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Saad Mtambule amewaasa Vijana kujiepusha na matendo ya uovu na uhalifu kwasababu hayo huondoa amani na upendo katika jamii.

Tamasha la Twenzetu kwa Yesu huandaliwa na Kanisa la KKKT kwa lengo la kuwaleta pamoja vijana kumsifu Mungu, kupata elimu ya fursa za mbalimbali za kiuchumi ili waweze kuendeleza na kukuza uchumi binafsi.








No comments:

Post a Comment