
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, leo Jumamosi Juni 21, 2025 ametembelea uwanja wa ndege wa Sumbawanga kukagua maendeleo ya ujenzi wake ambao unaendelea kwa kasi.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Mhandisi Besta amesema ujenzi wa uwanja huo umefikia asilimia 70, ambapo sehemu ya kuruka na kutua ndege (runway) tayari imekamilika, na kazi imebakia kwenye mita 15 tu kati ya jumla ya kilometa 1.7.
Ameongeza kwa kusema kuwa, baada ya kukamilisha sehemu hiyo, mkandarasi ataanza kazi ya kuweka alama (markings) kwenye runway, barabara za kuingilia ndege (taxiways), maegesho ya ndege (apron), pamoja na kuweka taa maalum (flight lights) kwa ajili ya usiku.
“Nimeridhishwa na maendeleo ya kazi hii na napenda kumpongeza msimamizi kutoka kampuni ya SMEC International kwa kusimamia kwa umakini na kuhakikisha kazi zinaendelea vizuri. Natarajia uwanja huu utakuwa tayari kutumika kuanzia mwezi Julai hadi Agosti,” alisema Besta.
Aidha, amemuelekeza mkandarasi kutoka kampuni ya BCEG pamoja na msimamizi SMEC International kuhakikisha wanakamilisha kazi ya kuweka alama za usalama kwa mujibu wa viwango na kuzingatia kanuni.
Uwanja wa ndege wa Sumbawanga unatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo kwa mkoa wa Rukwa kwa kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga na kuufungua kiuchumi.




No comments:
Post a Comment