Pwani yaanza vema mchezo wa wavu UMISSETA 2025 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, June 21, 2025

Pwani yaanza vema mchezo wa wavu UMISSETA 2025


Na OR-TAMISEMI, Iringa


Mkoa wa Pwani umeanza vyema mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) baada ya kuichapa Mkoa wa Mara kwa seti 3-1 katika mchezo wa mpira wa wavu wa wavulana uliochezwa kwenye viwanja vya Chuo cha Ualimu Kleruu, mkoani Iringa.

Katika mchezo huo wa kusisimua, Mara ilianza kwa kishindo kwa kushinda seti ya kwanza, lakini Pwani ilijibu mapigo kwa kurudisha seti ya pili na kuendelea kutawala hadi mwisho wa mchezo kwa ushindi wa seti 3-1.

Katika michezo mingine ya hatua ya makundi kwa upande wa wavulana, Kigoma iliibuka na ushindi wa seti 3-0 dhidi ya Shinyanga, wakati Ruvuma iliifunga Njombe kwa seti 3-0. Geita nayo ilionyesha ubabe kwa kuicharaza Songwe kwa seti 3-0, huku Kilimanjaro ikiibana Rukwa kwa seti 3-0. Wenyeji Iringa walikubali kipigo mbele ya Katavi kwa seti 3-0.


Kwa upande wa wasichana, Mara iliifunga Geita kwa seti 3-0, Kigoma ikaitandika Morogoro kwa seti 3-1, Singida ikaitupa nje Arusha kwa seti 3-0, Simiyu ikaiadhibu Dodoma kwa seti 3-0, na Lindi ikiitandika Rukwa kwa seti 3-0.

Akizungumza kuhusu mwenendo wa mashindano hayo, Kocha wa timu ya Mkoa wa Pwani, Bw. Damiano Mara, amesema kuwa mwaka huu ushindani umeongezeka kwa kiasi kikubwa tofauti na miaka ya nyuma, kwani sasa mikoa mingi imejiandaa vizuri na inashiriki kikamilifu katika mchezo wa wavu.

> "Tofauti na zamani ambapo idadi ya timu ilikuwa ndogo, mwaka huu karibu kila mkoa umeleta timu imara, na ushindani ni mkubwa sana. Hii inaonyesha maendeleo ya michezo nchini," alisema Kocha Damiano.

Mashindano ya UMISSETA yanaendelea kwa michezo mbalimbali huku vikosi vikiwania nafasi ya kusonga mbele katika hatua ya robo fainali.


No comments:

Post a Comment