OR - TAMISEMI
Serikali imefanikiwa kuajiri jumla ya Wataalam wa kada ya Ustawi wa Jamii 1,546, ambao kwa sasa wamepangiwa kazi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya kusaidia kukabiliana na tatizo la Afya ya Akili na Ustawi wa Jamii.
Hayo yamesema leo Juni 24 bungeni Jijini Dodoma katika kipindi cha maswali na majibu na Mhe. Dkt. Festo Dugange, Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Ofisi ya Rais – TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati akijibu swali la Mhe. Hawa Mwaifunga, Mbunge wa Viti Maalum.
Mhe. Mwaifunga alitaka kujua mpango wa Serikali kuajiri Wanasaikolojia ngazi ya Kata ili kusaidia kukabiliana na tatizo la Afya ya Akili.
Mhe. Dkt. Dugange ameongeza kuwa, hatua hiyo ya kuajiri wataalamu hao ni sehemu ya juhudi za kuboresha huduma za kisaikolojia kwa wananchi wenye uhitaji ambayo ni muhimu katika kuhakikisha kuwa huduma za afya ya kiakili zinapatikana kwa urahisi na kwa ufanisi kwa jamii nzima.
“Kwa mujibu wa Muundo wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wa mwaka 2022, huduma hizo hutoa msaada kwa watu wanaohitaji, zimepangwa kutolewa na Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe. Wataalam hawa wataanza kuelekeza huduma zao kupitia Makao Makuu ya Halmashauri na ngazi mbalimbali katika mamlaka husika”. alisema
Aidha, Serikali imesema itaendelea kuajiri wataalam wa kada ya Ustawi wa Jamii, kwa malengo ya kuhakikisha Halmashauri zilizokabiliwa na upungufu wa wataalam zinaweza kupata msaada wa kutosha katika kutoa huduma hizi muhimu kote nchini.
No comments:
Post a Comment