MIGOGORO YA ARDHI, MIRATHI NA NDOA YATAWALA HUDUMA ZA MSAADA WA KISHERIA KWA WANANCHI 231 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, June 24, 2025

MIGOGORO YA ARDHI, MIRATHI NA NDOA YATAWALA HUDUMA ZA MSAADA WA KISHERIA KWA WANANCHI 231


Migogoro ya ardhi, mirathi na ndoa ni miongoni mwa changamoto kubwa zilizotatuliwa kwa wananchi 231 waliotembelea Banda la Wizara ya Katiba na Sheria wakati wa Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika katika viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma kuanzia Juni 16 hadi 23, 2025.

Akizungumza kufungwa kwa maadhimisho hayo, Juni 23, 2025, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Abdulrahman Msham, alisema kuwa huduma zilizotolewa zilijumuisha msaada wa kisheria, elimu ya haki, uraia, utawala bora na utatuzi wa migogoro.

“Wananchi wengi waliohudumiwa walikumbwa na migogoro ya ardhi, ikifuatiwa na migogoro ya mirathi na ndoa. Hili linaakisi takwimu za Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia iliyotekelezwa kitaifa, ambapo migogoro ya ardhi imekuwa ikiongoza,” alieleza Msham.

Amefafanua kuwa migogoro ya mirathi inaendelea kuongezeka kutokana na warithi kugombania mali, hasa ardhi, jambo linalozua migogoro ya kifamilia ambayo mara nyingi huweza kuzuilika kwa elimu na usuluhishi wa awali.

Aidha, Bw. Msham amebainisha kuwa kupitia kampeni ya Mama Samia na maadhimisho haya, Wizara imeona changamoto hizo kama fursa ya kuboresha huduma na kuimarisha ushirikiano wa kisekta katika kutatua migogoro hiyo kwa manufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla.

“Lengo letu ni kuwa na Tanzania salama yenye wananchi wanaoifahamu Katiba na sheria na wanaoziheshimu kwa maendeleo ya taifa,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Msham ametangaza kuwa Wizara ya Katiba na Sheria itashiriki Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa yatakayofanyika kuanzia Juni 28, 2025 katika viwanja vya Sabasaba, Temeke jijini Dar es Salaam, ambapo itaendelea kutoa huduma za msaada wa kisheria pamoja na elimu ya haki, uraia na utawala bora kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment