SIMBACHAWENE AIPONGEZA WIZARA YA SHERIA KWA KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, June 17, 2025

SIMBACHAWENE AIPONGEZA WIZARA YA SHERIA KWA KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA



Na OKULY JULIUS, DODOMA


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene, ameipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuendeleza juhudi za kutatua migogoro katika jamii kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia.

Amesema juhudi hizo zimechangia kupunguza malalamiko na migogoro katika jamii, hali iliyosaidia kuimarisha utulivu na kurahisisha maendeleo ya wananchi.

Simbachawene ametoa pongezi hizo Juni 17, 2025 jijini Dodoma alipokuwa akitembelea banda la Wizara hiyo katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park.

“Ukitaka kuhakikisha kuwa maendeleo yapo ni lazima tuhakikishe hakuna migogoro. Kama ni kesi tayari zilishakuwepo mahakamani, lakini jitihada kubwa mmezifanya na sasa mmechochea amani na upendo katika jamii,” amesema Simbachawene.

Ametaka jitihada hizo ziendelezwe ili kusaidia jamii kuondokana na migogoro inayoweza kuhatarisha amani na mshikamano wa kitaifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Mbaraka Stambuli, amesema Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia imelenga kuwasaidia wananchi wasioweza kumudu gharama za mawakili au kuandaa nyaraka za kisheria.

“Kampeni hii inahakikisha kila mwananchi anapata haki yake. Mpaka sasa tumeweza kuwafikia wananchi milioni tatu Tanzania Bara na Visiwani, na tunatarajia kuja na awamu ya pili ya kampeni hii,” amesema Mbaraka.




No comments:

Post a Comment