
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea na zoezi la kulifanya Jiji la Dodoma kuwa la kijani kwa kupanda miti 150,000 kwenye barabara nne za mzunguko wa nje kupitia mradi wa Kijanisha Jiji la Dodoma (Green Solution Project - GSP) ambao ni msaada kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Mratibu wa mradi huo kutoka TANROADS Bw. Julius Luhuro amesema mradi huu wa upandaji wa miti ni wa kimkakati, ambao umedhamiria kulifanya Jiji la Dodoma liweze kupambana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Bw. Luhuro amesema mradi huu unasimamiwa na TANROADS inayoshirikiana na taasisi nyingine zikiwemo Jiji la Dodoma, Taasisi ya Utafiti wa Misitu (TAFURU), taasisi ya usimamizi wa Misitu (TFS), Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) na Wakala wa Usimamizi wa Majengo.
Amesema lengo la msingi la mradi huu ni kuongeza nguvu ya serikali katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
“Zoezi hili linafanywa kwa kipindi cha miaka mitatu na Kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kambi ya Makutupora, na hii barabara yetu itakuwa ya mfano kwa kuwa na ukanda wa kijani kwa kupandwa hii miti na tutaweza kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuongeza uoto wa kijani utakaokuwa na mchango mkubwa wa kupunguza gesi joto,” amesema Bw. Luhuro.
Hatahivyo, amesema zoezi hilo la upandaji miti ya aina mbalimbali ikiwemo ya matunda lilianza mwezi Novemba mwaka 2024, ambapo hadi sasa tayari miti 35,000 imepandwa kwenye barabara ya mzunguko wa nje ya jiji la Dodoma, ambalo kwa ujumla lina Kilometa 112.
Amesema kutokana na ukame tayari vimechimbwa visima 11 kwa ajili ya kutumika kumwagilia miti hiyo, ambapo pia kutatumika njia ya umwagiliaji wa matone.
Kwa upande wake Meneja wa Mazingira na Jamii wa TANROADS, Bi. Zafarani Madayi taasisi hiyo imekuwa na zoezi endelevu la upandaji wa miti kwenye miradi mbalimbali ya barabara, ili kuweka mazingira katika hali ya usafi.
Halikadhalika Bi. Madayi amewaasa wananchi kuacha kutupa takataka aina ya plastiki ambazo ni moja ya chanzo cha kuziba kwa mifereji kipindi cha mvua, na kusababisha maji kuharibu barabara.
Naye Operesheni Kamanda wa zoezi la upandaji miti kutoka Kikosi cha JKT Makutupora Kapteini Kosam Mwangupili amesema zoezi hilo la upandaji wa miti lilianza kilometa 20 eneo la Nala hadi Mahomanyika kwa kupandwa miti 18,000 ya matunda, mikrismas, miti maji, midodoma, miakasha, miarubaini, mijohoro, michikichi na kivuli.
Kapteini Mwangupili amesema wanakabiliwa na changamoto kubwa ya wananchi kupitisha mifugo kwenye maeneo yaliyopandwa miti, ambapo mingi imekuwa ikiliwa na kukanyagwa na wanyama hao hususan ng’ombe na mbuzi.
“Nipende kutoa wito kwa wananchi kuilinda hii miti serikali imetoa fedha nyingi, na hii miti ikikuwa itatunufaisha wote kwa kuweka mazingira katika hali nzuri, na pia kutoa matunda kwa kuwa ipo miti mingi ya matunda kama maembe, pia wale wwenye kung’oa hususan miti ya miembe na kwenda kupanda majumbani mwao waachez kufanya hivyo,” amesisitiza Afande Mwangupili.
Kwa upande wake Mhandisi Chacha Marwa kutoka Wizara ya Ujenzi kitengo cha Usalama na Mazingira, amesema mradi huu wa upandaji miti unafaida kubwa ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ambapo imeelekezwa kwenye sheria ya mazingira ya 2024 kifungu cha 75 na sheria ya barabara kifungu cha 30 kinaeleza uhifadhi na usimamizi wa mazingira.
“Pia kanuni ya mwaka 2009 na sera ya mazingira ya mwaka 2021 nayo inaelezea kuhusiana na mabadiliko ya tabianchi, na hii tunatekeleza makubalianoi ya Paris sehemu ya sita (6) ya upunguzaji wa gesijoto,” amesema Mha. Marwa.
Katika hatua nyingine TANROADS kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi, leo tarehe 4 Juni, 2025 wamepanda miti takribani 150 kwenye maeneo ya Veyula ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani inayofanyika jijini Dodoma kuanzia Juni 1 na itafikia kilele Juni 5, 2025.






No comments:
Post a Comment