
Tanzania kupitia Mfumo wa e-Mrejesho toleo la pili (e-MrejeshoV2) imeibuka mshindi katika kipengele cha Serikali Mtandao, kwenyeTuzo za Mkutano wa Dunia wa Jumuiya ya TEHAMA mwaka 2025 (World Summit on the Information Society -WSIS 2025).
Utoaji wa tuzo za WSIS umefanyika Julai 7 katika mkutano wa Tukio la Ngazi ya Juu la Jukwaa la WSIS+20 (WSIS+20 Forum High-Level Event), unaofanyika mjini Geneva USWIS kuanzia tarehe 7 hadi 11 Julai mwaka huu. Mhe. Jerry Silaa (Mb) Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari alipokea tuzo hiyo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Tuzo hizo ambazo huratibiwa na Shirika la Mawasiliano la Umoja wa Mataifa (International Telecommunications Union – ITU) zinalenga kutambua na kuchochea miradi bunifu, inayotumia TEHAMA katika kuchangia maendeleo endelevu duniani.
Akieleza kuhusu ushindi huo, Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Bi. Subira Kaswaga amesema, Mfumo wa e-Mrejesho toleo la pili (V2), umeibuka mshindi wa tuzo hiyo katika kipengele cha Serikali Mtandao (e-Government AL C7), kati ya mifumo 360 ya TEHAMA iliyofuzu hatua ya awali ya mchujo kutoka kwa zaidi ya maombi 1000 ya mifumo ya kidijitali yaliyowasilishwa kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Baada ya mchujo wa awali, mfumo wa eMrejesho ulifanikiwa kuingia kundi la tano bora kupitia taarifa iliyopokelewa na e-GA kutoka ITU kwa njia ya baruapepe, hii ilikuwa ni hatua muhimu kwa e-GA na kudhihirisha namna Watanzania walivyoshiriki kupiga kura, na kuwezesha mfumo huo kuingia katika tano bora.
“Nifuraha kubwa kuona wananchi wameweza kuitikia wito na kuwa wazalendo kwa kufanya kazi kubwa ya kuhakikisha wanapiga kura kwa wingi na hatimaye tuzo imekuja nyumbani, kwa niaba ya e-GA tunawashukuru sana” amesema Bi. Subira.
Mfumo wa e-Mrejesho (V2) umesanifiwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), ukiwa umeboreshwa kwa kutumia teknolojia ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence - AI) katika kukusanya maoni ya wananchi. Mfumo huu unasimamiwa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Mfumo wa eMrejesho unapatikana kwa njia tatu ambazo ni kupitia simu ya mkononi kwa kubofya *152*00# na kisha kuchagua namba 8 na kisha namba 2 na kisha kufuata maelekezo. Pia, kupitia simu janja kwa kupakua Aplikesheni tumizi (Mobile App) ya e-Mrejesho inayopatikana kwenye ‘Play Store na Apps Store’, na kwa njia ya Tovuti ya e-mrejesho.gov.go.tz.



No comments:
Post a Comment