
Na WMJJWM – Mwanza
Maafisa Maendeleo ya Jamii nchini wametakiwa kutoa elimu kwa vikundi vya wanawake, vijana, watu wenye ulemavu na wazee ili waweze kushiriki kikamilifu kwenye fursa ya asilimia 30 ya ununuzi wa umma.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu Juni 30, 2025 jijini Mwanza wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Maafisa Maendeleo ya Jamii kuhusu namna ya kuongeza ushiriki wa makundi maalum katika zabuni za umma.
Dkt. Jingu amesema katika utekelezaji wa matakwa ya Sheria ya Manunuzi hakuna mtu anayepaswa kuachwa nyuma katika mpango wa ununuzi wa umma wa asilimia 30 hivyo Maafisa Maendeleo ya Jamii wanapaswa kuhakikisha wanatoa hamasa kwa makundi hayo.
“Hatupaswi kukaa tu, lazima tuhakikishe vikundi hivi vinawezeshwa, vinaunganishwa na mifumo ya zabuni, na vinanufaika na fursa zilizopo,” amesema Dkt. Jingu.
Aidha, Dkt. Jingu amezitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha zinaanzisha na kusajili angalau vikundi 20 vinavyokidhi vigezo vya kushiriki zabuni shindani na kuelekeza Maafisa Maendeleo ya Jamii kuhakikisha wanavisaidia vikundi hivyo kwa kuwaunganisha moja kwa moja na wadau wa manunuzi ili wapate taarifa, mafunzo na fursa zinazohitajika.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Mipango Mkoa wa Mwanza, Henry Mwaijenga, amesema mafunzo hayo ni muhimu na kuwaomba Maafisa Maendeleo ya Jamiii kuhakikisha elimu waliyoipata wanaitumia kuwafundisha wanavikundi ili viweze kutumia fursa hizo kujikwamua kiuchumi.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Juliana Kibonde, amesema lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwahamasisha Maafisa Maendeleo ya Jamii nchini kuelimisha na kusaidia urasimishaji wa vikundi vya makundi maalum ili viweze kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ununuzi wa umma.






No comments:
Post a Comment