MAPATO YA UVUVI MWANZA YAFIKIA BILIONI 8.2, SAMAKI WAVUKA MIPAKA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, July 16, 2025

MAPATO YA UVUVI MWANZA YAFIKIA BILIONI 8.2, SAMAKI WAVUKA MIPAKA

MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda,akizungumza leo, Julai 16, 2025, na waandishi wa habari jijini Dodoma, kuhusu mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan. 
MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda,akizungumza leo, Julai 16, 2025, na waandishi wa habari jijini Dodoma, kuhusu mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.


Na Okuly Julius _ DODOMA 


MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, amesema Mkoa wa Mwanza umeendelea kunufaika kwa kiasi kikubwa na mageuzi katika sekta ya uvuvi na ufugaji wa samaki, hasa kupitia matumizi ya teknolojia ya kisasa katika uzalishaji na usindikaji wa mazao ya samaki.

Akizungumza leo, Julai 16, 2025, na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita, Mhe. Mtanda amesema idadi ya vizimba vya kufugia samaki (fish cages) imeongezeka kutoka 1,664 mwaka 2020 hadi kufikia 2,715 mwaka 2025, sawa na ongezeko la vizimba 1,051.

Ameeleza kuwa katika mwaka 2024 pekee, zaidi ya tani 43,657.6 za minofu ya samaki zilichakatwa, huku tani 81,812 zikisafirishwa nje ya nchi kupitia Uwanja wa Ndege wa Mwanza, jambo linalodhihirisha mchango wa sekta hiyo katika kukuza uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.

Aidha, usafirishaji wa mabondo ya samaki kwenda nje ya nchi umeongezeka kutoka kilo 431,721 mwaka 2020 hadi kilo 495,448 mwaka 2024, ongezeko la kilo 63,727.

Mkuu huyo wa mkoa pia amebainisha kuwa idadi ya mabwawa ya kufugia samaki imeongezeka kutoka 286 mwaka 2020 hadi 531 mwaka 2025, ikiwa ni ongezeko la mabwawa 245.

“Haya mafanikio ni ushahidi wa dhahiri kuwa juhudi za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha uchumi wa buluu na sekta ya uvuvi zimezaa matunda. Mapato yatokanayo na shughuli za uvuvi yameongezeka kutoka shilingi bilioni 4.4 mwaka 2020 hadi kufikia bilioni 8.2 mwaka 2025,” amesema Mhe. Mtanda.

Amesisitiza kuwa Mkoa wa Mwanza utaendelea kuhamasisha uwekezaji, utafiti, na matumizi ya teknolojia ili kuhakikisha wananchi, wakiwemo wavuvi wadogo, wafugaji wa samaki, na wafanyabiashara wa dagaa, wananufaika ipasavyo na rasilimali za Ziwa Victoria.

No comments:

Post a Comment