
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akisalimiana na baadhi ya watumishi wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma mara baada ya kuwasili katika jengo jipya la ofisi hiyo lililopo eneo la Tambukareli jijini Dodoma.

Baadhi ya watumishi wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (Hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati alipotembelea jengo jipya la ofisi hiyo iliyopo eneo la Tambukareli jijini Dodoma.

Mwonekano wa Jengo jipya la Sekretarieti ya Ajira lililopo eneo la Tambukareli jijini Dodoma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza na Viongozi na Watumishi ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma (hawapo pichani) jijini Dodoma wakati alipotembelea jengo jipya la ofisi hiyo iliyopo eneo la Tambukareli jijini Dodoma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akifurahia jambo na Naibu Waziri wa ofisi hiyo Mhe. Deus Sangu mara baada ya Waziri huyo kuwasili katika jengo jipya la ofisi ya Sekretarieti ya Ajira iliyopo eneo la Tambukareli jijini Dodoma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akifurahia jambo na Viongozi wa ofisi yake na Watendaji wa ofisi ya Sekretarieti ya Ajira wakati wakikagua ukumbi wa kufanyia usaili kwenye jengo jipya la ofisi hiyo iliyopo eneo la Tambukareli jijini Dodoma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (wakwanza kushoto) akisalimiana na Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Bw. Mick Kiliba (wakwanza kulia) wakati Waziri huyo alipotembelea jengo jipya la ofisi ya Sekretarieti ya Ajira iliyopo eneo la Tambukareli jijini Dodoma.
Na. Veronica Mwafisi-Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene ametembelea jengo jipya la Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma na kutoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha rasilimali fedha za ujenzi wa jengo hilo na maelekezo ambayo amekuwa akiyatoa mara kwa mara ya kuboresha shughuli za taasisi hiyo ikiwemo mchakato mzima wa ajira nchini.
Akizungumza na Watumishi wa Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma leo mara baada ya kufika katika Ofisi hiyo iliyopo eneo la Tambukaleri jijini Dodoma, Mhe. Simbachawene amesema mahitaji ni mengi lakini Rais aliona ni muhimu pamoja na mambo mengine suala la ajira likapewa kipaumbele hasa kwa kuwa na jengo lake katika uendeshaji wa mchakato wa ajira.
Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita hasa Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo mbalimbali na utashi wake binafsi wa kutuwezesha kuwa na jengo hili na majengo mengine yaliyo chini ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, haya yote yasingewezekana kwa sababu mahitaji ni mengi Mhe. Simbachawene ameongeza.
Mhe. Simbachawene ameipongeza Bodi na Menejimenti ya Ofisi hiyo kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa jengo hilo na wote waliohusika ikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuhakikisha jengo la ofisi hiyo linakamilika kwa ustadi.
“Lengo langu leo ni kuangalia jengo, kwa kweli jengo limejengwa kwa ustadi mkubwa sana, niwapongeze wataalam wote waliohusika katika ujenzi na waliosimamia, jengo lina mvuto na thamani ya fedha inaonekana. Mhe. Simbachawene amesisitiza.
Aidha, Mhe. Simbachawene amezungumzia suala la mchakato wa ajira kufanyika mikoani na kuchukua barua za ajira mikoani kuwa ni maelekezo ya Rais ambayo alielekezwa ili kupunguza gharama na muda wa wasailiwa.
Maelekezo yote ya kuboresha mchakato wa ajira ambayo nilikuwa nikiyatoa kwa Bodi na Menejimenti nilikuwa nikipewa na Rais, hivyo hatuna budi kumshukuru kwa maelekezo yake yenye kujenga” Ameongeza.
Mhe. Simbachawene amewasisitiza watumishi wa Ofisi hiyo kuendelea kusimamia kikamilifu zoezi la usaili wa ajira na kuwa makini ili wenye sifa wapate ajira kwa haki bila upendeleo.
Naye Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu ameipongeza Sekretarieti ya Ajira kwa kuwa wepesi kupokea maelekezo mbalimbali yaliyokuwa yakitolewa na viongozi ili kuboresha utendaji kazi wa taasisi hiyo.
Amewataka watumishi wa ofisi hiyo kutumia ofisi hiyo mpya kama chagizo la morali ya kufanya kazi.
“pongezi kwa ofisi kuwa na jengo lake na Mhe. Simbachawene kwa maelekezo, usimamizi na uongozi vimeonekana kwa vitendo. Mimi ni shahidi, nimekuwa nikipokea maelezo yako ya kushughulikia changamoto za taasisi hii. Mhe. Sangu amesema
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wajumbe wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Bibi Sofia Kaduma amemshuru Waziri Simbachawene kwa miongozo na maelekezo ambayo amekuwa akiyatoa kwa Bodi na Menejimenti hiyo ambayo yameongeza ufanisi na kuleta tija kwa taifa.
Kwa upande wake Katibu wa Sekretarieti ya Ajira Katika Utumishi wa Umma, Bwana Mick Kiliba amesema utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa jengo la ofisi hiyo ulianza tarehe mwezi Aprili, 2022 kupitia Mshauri Elekezi wa Mradi (Chuo Kikuu cha Ardhi) kupitia Kampuni ya ARU Built Environment Consulting Company Limited (ABECC).
No comments:
Post a Comment