MMOMONYOKO WA MAADILI CHANZO CHA RUSHWA SERIKALINI - CHALAMILA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, July 30, 2025

MMOMONYOKO WA MAADILI CHANZO CHA RUSHWA SERIKALINI - CHALAMILA


Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Crispin Chalamila akizungumza na waandishi wa habari Julai 30,2025 jijini Dodoma, baada ya kufungua kikao kazi cha siku mbili cha kubadilishana uzoefu kuhusu maadili na utawala bora kati ya taasisi simamizi za maadili ya utendaji na mamlaka za maadili ya kitaaluma.


Na OKULY JULIUS, OKULY BLOG - DODOMA


Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Crispin Chalamila, amesema mmomonyoko wa maadili katika ngazi ya familia ndio chanzo kikuu cha kuenea kwa vitendo vya rushwa miongoni mwa watumishi wa umma na taasisi mbalimbali.

Chalamila ameyasema hayo jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha siku mbili cha kubadilishana uzoefu kuhusu maadili na utawala bora kati ya taasisi simamizi za maadili ya utendaji na mamlaka za maadili ya kitaaluma.

“Kaulimbiu ya kikao hiki ni ‘Mmomonyoko wa maadili ni chanzo kimojawapo cha rushwa, tushirikiane kuimarisha maadili.’ Hii ni kutokana na ukweli kwamba ukosefu wa maadili ndio chanzo kikuu cha matatizo yote, ikiwemo rushwa.”ameeleza Chalamila

Ameongeza kuwa hata mtumishi mwenye uwezo mkubwa kitaaluma, iwapo hana maadili mazuri, ni rahisi kujihusisha na vitendo viovu kama kuomba au kupokea rushwa ili kutoa huduma.

Kwa mujibu wa Chalamila, usimamizi wa maadili ya utumishi wa umma ni jukumu la kisheria chini ya Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kwa mujibu wa kifungu cha 8(3)(e) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298.

“Jukumu hili linahusisha pia taasisi simamizi za maadili pamoja na mamlaka za maadili ya kitaaluma, ambao sisi sote tumekutana hapa. Ni wajibu wetu kuona kwamba tunadhibiti mmomonyoko wa maadili kwa pamoja,” alisema.

Chalamila amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa pamoja katika kutengeneza mikakati ya kuimarisha maadili ya utendaji na kitaaluma, ili kudhibiti vitendo vya rushwa kwa lengo la kuongeza uwajibikaji na ufanisi katika utoaji huduma kwa wananchi.

“Ninatoa rai tuendelee kushirikiana na kuwekeza kwenye mikakati inayolenga kuimarisha utendaji wa wataalamu wetu, kwa azma ya kuifikia ndoto ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwa na utumishi wa umma unaowajibika kwa hiari na kwa maslahi ya wananchi,” aliongeza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Maadili kutoka Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Felister Shuli, alisema utafiti wa mwaka 2021 uliofanywa na ofisi hiyo unaonesha kuwa maadili ya utumishi wa umma yanaendelea kuimarika.

“Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa wananchi wameanza kuripoti ukiukwaji wa maadili, na pia watumishi wengi wa umma sasa wanazingatia misingi ya maadili kazini. Hata hivyo, bado kuna changamoto katika ngazi ya familia ambazo zinahitaji kushughulikiwa,” alisema Shuli.

Kikao hicho kimehudhuriwa na taasisi mbalimbali zikiwemo TAKUKURU, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA), Bodi ya Wakandarasi (CRB), na Baraza la Wakunga na Wauguzi Tanzania (TNMC).



No comments:

Post a Comment