
Na Mwandishi Wetu - Dar es Salaam.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi leo tarehe 07 Julai, 2025 ametembelea Banda Jumuishi la Ofisi ya Waziri Mkuu lililopo katika Maonesho ya 49 ya Biashara (SABASABA) yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.
Katika banda hilo, Dkt. Mwinyi ameona mifumo mbalimbali ikiwemo Mfumo wa Ramani za Vihatarishi vya Maafa Vinavyotokana na Mabadiliko ya Tabianchi umeandaliwa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa masharti ya kifungu cha 31(2)(a) cha Sheria ya Usimamizi wa Maafa, Sura ya 242 kinachotoa wajibu kwa Wizara, Idara, taasisi za Serikali, Tawala za Mikoa, na mamlaka za Serikali za mitaa kujumuisha katika mipango na bajeti zao hatua za kuzuia na kupunguza madhara ya majanga na kujiandaa kukabiliana na maafa.
Mfumo huo unatoa taarifa za vihatarishi vya maafa kwa kutumia teknolojia ya mifumo ya taarifa za kijiografia zinazowezesha utambuzi wa maeneo yaliyo katika hatari zaidi ya kuathirika na majanga yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi kama mafuriko, ukame na ongezeko la joto. Kwa kuzingatia viashiria vya kijamii, kiuchumi, kimazingira na kiteknolojia.
Lengo la mfumo huo ni kusaidia taasisi za serikali, sekta binafsi, mashirika ya maendeleo na wadau wengine kutumia ipasavyo ramani hizo katika upangaji na utekelezaji wa mipango na mikakati katika uendelezaji wa miundombinu, usimamizi wa matumizi ya ardhi na shughuli za kiuchumi.
Aidha, Dkt. Mwinyi ameelezwa kuhusu mfumo wa taarifa ya haraka dhidi ya moto, mfumo unaolenga kushughulikia changamoto ya ucheleweshwaji wa taarifa kuwafikia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kutokana sababu mbalimbali ikiwemo kutofahamu namba ya dharura na taharuki pindi tukio la moto linapotokea, vilevile katika maeneo yenye vikwazo vya matumizi ya simu za mkononi kama vile mashuleni na magereza.
Mfumo huo umeunganishwa moja kwa moja na mtungi wa kuzimia moto, ambapo mara mtungi unapochukuliwa kwa ajili ya kudhibiti moto, mfumo hutuma taarifa ya tahadhari kwa njia ya simu na ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) ukionesha eneo la tukio kwa Jeshi la Zimamoto na wadau husika bila kuhitaji uingiliaji wa binadamu.
Vilevile, Rais Mwinyi ameelezwa kuhusu Mfumo wa Kitaifa wa Taarifa za Watu Wenye Ulememavu ambapo ni programu ya kielektroniki inayojumuisha Usajili wa Watu wenye ulemavu, Hifadhi salama ya Taarifa za Watu wenye ulemavu pamoja na Kuhamisha Taarifa za Watu wenye Ulemavu.
Aidha, faida za mfumo huo unalenga kupunguza gharama za usafiri na vifaa kwa ajili ya usafiri, kutoa takwimu sahihi zinazosaidia serikali, kupanga na kutekeleza sera kwa ufanisi na kuongeza ujumuishaji wa watu wenye ulemavu kwenye huduma za kijamii na maendeleo.
Rais Mwinyi ametembelea banda hilo kama Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Saba Saba yanayofanyika katika viwanja vya Sabasaba, Kilwa Road, Jijini Dar es Salaam.









No comments:
Post a Comment