
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imepongezwa kwa hatua kubwa katika kuwekeza kwenye elimu ya msichana kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.
Pongezi hizo zimetolewa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne na Mwenyekiti wa Bodi ya Global Partnership for Education (GPE) Duniani, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, alipofanya ziara katika Shule ya Sekondari Kibasila jijini Dar es Salaam, akiwa ameambatana na wawakilishi wa Jakaya Mrisho Kikwete Foundation (JMKF), Malala Fund na GPE.
Dkt. Kikwete amesema juhudi za serikali zimechangia ongezeko la ufaulu, idadi ya wanafunzi wanaojiunga na elimu ya juu, pamoja na mazingira bora ya kujifunzia kwa watoto wote, hususan wasichana.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. QS Omari Kipanga amesema mageuzi ya mitaala yanalenga kujenga mazingira salama, jumuishi na ya kisasa, akibainisha kuwa teknolojia ya kidijitali na matumizi ya akili bandia (AI) yameingizwa kwenye mitaala ili kuwajengea wanafunzi maarifa yanayohitajika kwenye soko la sasa.
Naye Malala Yousafzai, Mwanzilishi wa Malala Fund, amepongeza Tanzania kwa kujitahidi kuwawezesha wasichana kupata elimu na kutoa wito kwa jamii kuhakikisha kuwa hakuna msichana anayekatisha masomo kwa sababu ya changamoto za kijamii au kiuchumi.













No comments:
Post a Comment