
Na Mwandishi Wetu, SINGIDA
Ushirikiano wa NSSF na Mahakama Chachu ya Mafanikio Katika Hifadhi ya Jamii rasmi katika kikao kazi kati ya Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mhe. Augustine Mwarija – Jaji wa Mahakama ya Rufani aliye mwakilisha Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju – amesisitiza kuwa ushirikiano imara kati ya NSSF na wadau, hasa Mahakama, umekuwa kichocheo kikubwa cha mafanikio ya Mfuko huo. Amesema kuwa ushirikiano huu unatoa nafasi ya kujadili changamoto kwa pamoja, kubadilishana uzoefu na kubuni njia bora za kuimarisha huduma kwa wanachama.
Mhe. Mwarija alipongeza waandaaji wa kikao kazi hicho kilichoandaliwa na Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) kwa kushirikiana na NSSF, na kusema kuwa kikao hiki ni utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania (2021–2025), hususan nguzo ya tatu inayolenga ushirikishwaji wa wadau katika utoaji wa haki. Aliongeza kuwa changamoto kama za mirathi zinahitaji kushughulikiwa kwa pamoja kwa kuweka mifumo ya pamoja inayotambua wategemezi na kuharakisha utoaji wa haki.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba alieleza kuwa tangu mwaka 2018 Serikali ilipofanya maboresho makubwa ya sheria, NSSF imekuwa chombo pekee kinachotoa huduma za hifadhi ya jamii kwa sekta binafsi na waliojiajiri. Mwaka 2024, kupitia mabadiliko ya Sheria ya NSSF (Sura ya 50), wanachama sasa wanaweza kuchangiwa na zaidi ya mwajiri mmoja, vipindi vya uchangiaji vya zaidi ya miaka 60 vinazingatiwa, adhabu ya kuchelewesha michango imepunguzwa kutoka asilimia 5 hadi 2.5, na waliojiajiri sasa wanaweza kujiunga kupitia mpango wa lazima (mandatory).
Bw. Mshomba alieleza kuwa thamani ya Mfuko imeongezeka kwa kiasi kikubwa kutoka Shilingi trilioni 4.8 mwaka 2021 hadi kufikia Shilingi trilioni 9.6 hadi kufikia Juni 2025, ikiwa ni ongezeko la asilimia 98. Aidha, michango ya wanachama imeongezeka kutoka trilioni 1 hadi trilioni 2.16, huku mapato ya uwekezaji yakipanda kutoka Shilingi bilioni 527.1 hadi bilioni 543.5.
Mafanikio mengine yaliyoelezwa ni pamoja na ongezeko la thamani ya vitega uchumi vya Mfuko kufikia trilioni 8.2 kutoka trilioni 7.4. Vilevile, mafao ya wanachama yaliyolipwa yamefikia Shilingi bilioni 947.2 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ikilinganishwa na Shilingi bilioni 884.8 mwaka uliotangulia, ongezeko la asilimia 7. NSSF pia inalenga kulipa mafao ndani ya saa 24 pindi mwanachama anapostaafu, hatua inayowezekana kupitia maboresho ya TEHAMA ambapo kwa sasa huduma za Mfuko zinatekelezwa kwa asilimia 90 kwa njia ya kidijitali.
Katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 2025, NSSF imefikisha wanachama wachangiaji 1,816,026 kutoka 1,358,882 mwaka uliotangulia, ongezeko la asilimia 19. Ongezeko hili limetokana na mabadiliko ya sheria ambayo sasa yanamruhusu kila Mtanzania analiye katika shughuli za kujiajiri kujiunga na hifadhi ya jamii, hivyo kuimarisha uhakika wa kipato kwa Watanzania wote kwa kuwa na akiba ya uhakika na kuwa mnufaika wa hifadhi ya jamii muda utakapofika. Bw. Mshomba amesema pamoja na mambo mengine, mazingira mazuri ya kisera yaliyoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yamechangia mafanikio ya Mfuko.
Pamoja na mafanikio haya, changamoto bado zipo. Bw. Mshomba alibainisha kuwa baadhi ya waajiri hawawasilishi michango kwa wakati au huwasilisha kwa kiwango kidogo tofauti na kiasi halisi wanachowalipa wafanyakazi wao. Hata hivyo, elimu inaendelea kutolewa kwa waajiri na wafanyakazi kuhusu umuhimu wa hifadhi ya jamii,kuwasilisha michango sahihi na kwa wakati.
Mwenyekiti wa TMJA Tawi la Mahakama ya Rufani, Mhe. Shabani Ally Lila ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, aliishukuru NSSF kwa kuandaa kikao kazi hicho ambacho kimelenga kushirikisha wadau muhimu katika kuhakikisha haki za wanachama zinalindwa. Alisema kikao kazi hicho ni jukwaa muhimu la kuimarisha ushirikiano na kuhakikisha mafao ya wastaafu yanalipwa kwa wakati na haki.
Kwa upande wake, Mhe. Bupe Abonike Kibona – Hakimu Mkazi na Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mahakama ya Rufani – alisema kuwa kikao kazi hicho kimewapa maarifa ya kina kuhusu taratibu za NSSF, jambo litakalosaidia mahakama kushughulikia kesi za hifadhi ya jamii kwa haraka na kwa usahihi zaidi. Aliongeza kuwa mpango wa Hifadhi Scheme wa NSSF ni hatua chanya inayowawezesha Watanzania wote kujiunga na kunufaika na mafao mbalimbali ya hifadhi ya jamii.
Kikao kazi kati ya TMJA na NSSF kilichofanyika mkoani Singida, kimehudhuriwa na Majaji wa Mahakama ya Rufani, Wasajili, Mahakimu, pamoja na watendaji wa NSSF, kikiongozwa na kaulimbiu isemayo “Utoaji Haki kwa Wakati kwa Ustawi wa Hifadhi ya Jamii.”













No comments:
Post a Comment