TANZANIA YAIVUTIA GAMBIA MAGEUZI YA ELIMU. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, July 5, 2025

TANZANIA YAIVUTIA GAMBIA MAGEUZI YA ELIMU.



Na Okuly Julius DODOMA


WAZIRI wa Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia na Utafiti kutoka Serikali ya Gambia, Prof. Pierre Gomez, ameongoza ujumbe mkubwa kutoka nchini humo uliowasili Tanzania kwa ajili ya kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu namna Tanzania ilivyotekeleza mageuzi katika sekta ya elimu, hususan kwenye mafunzo ya amali.

Akizungumza leo Julai 5, Mtumba Jijini Dodoma, mara baada ya mazungumzo na ujumbe huo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wa Tanzania, Prof. Adolf Mkenda, amesema ujumbe kutoka Gambia umevutiwa na hatua kubwa zilizopigwa na Tanzania katika kuboresha mafunzo ya amali kwa vitendo.

Prof. Mkenda alieleza kuwa wamekubaliana kuandaa makubaliano ya ushirikiano yatakayowezesha kubadilishana wanafunzi na wakufunzi kati ya nchi hizo mbili, hususan katika fani za ufundi stadi na teknolojia. Ushirikiano huo unatarajiwa kuimarisha uwezo wa vijana katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake, Prof. Gomez amesema taasisi mbalimbali za kimataifa zinazoshirikiana na Serikali ya Gambia ndizo zilizowashauri kuitembelea Tanzania ili kujifunza kutoka kwenye mafanikio yaliyopatikana kupitia mageuzi ya sekta ya elimu, akisisitiza kuwa Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa barani Afrika katika kuwekeza kwenye elimu ya vitendo na teknolojia.

Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Gambia kuboresha mfumo wake wa elimu kwa kutumia mifano bora ya utekelezaji wa sera, mifumo na mbinu za ufundishaji kutoka nchi marafiki.
















No comments:

Post a Comment