
Na Okuly Julius ,OKULY BLOG, DODOMA
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeitaka Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) kufanya tafiti za kina katika baadhi ya mikoa inayoonekana kuwa nyuma katika stadi za msingi za kusoma, kuandika na kuhesabu ili kuwezesha maboresho ya kitaalamu na kimkakati katika maeneo hayo.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hussein Omary, wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Maafisa wa Magereza pamoja na wawezeshaji wa programu ya Kisomo yaliyofanyika jijini Dodoma.

"Ni muhimu sasa TEWW kufanya tafiti katika maeneo ambayo yanaonekana kuwa nyuma kielimu, ili kubaini sababu na kuandaa mikakati ya haraka na madhubuti ya kuboresha stadi za msingi kwa wananchi."
Kwa upande wake, Prof. Philipo Sanga, Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wawezeshaji wa Kisomo ili kuongeza ufanisi katika matumizi ya mbinu shirikishi na bunifu za ufundishaji.
"Tunaamini kupitia mafunzo haya, wawezeshaji wetu wataweza kuleta mabadiliko chanya kwa kutumia mbinu stahiki zinazokidhi mahitaji ya walengwa wetu."

Naye Mkuu wa Gereza la Isanga, ACP William Selethaa, ambaye ni miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo, amesema elimu ya watu wazima inapaswa kuendelea kuimarishwa zaidi kwa kuwa imekuwa msaada mkubwa kwa wafungwa wanaopatiwa stadi mbalimbali gerezani.
"Tunaona mafanikio makubwa kwa wafungwa wanaopata elimu kupitia programu hizi. Wengi wanatoka gerezani wakiwa wamewezeshwa na stadi muhimu za maisha."
Kwa mujibu wa historia, elimu ya watu wazima ilianzishwa rasmi nchini takribani miaka 50 iliyopita na imechangia kwa kiasi kikubwa kuwaongezea Watanzania maarifa na stadi za amali, hivyo kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kijamii.
Miongoni mwa majukumu ya msingi ya TEWW ni pamoja na kuandaa walimu na wasimamizi wa elimu ya watu wazima pamoja na elimu nje ya mfumo rasmi, ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata fursa ya msingi ya kujifunza na kuboresha maisha yake.








No comments:
Post a Comment