
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Kenani Laban Kihongosi,akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu Mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika
Mkoani huo.
Na Okuly Julius ,OKULY BLOG, DODOMA
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeleta mageuzi makubwa ya maendeleo katika Mkoa wa Arusha kwa kipindi cha miaka minne (2021–2025), ambapo jumla ya Shilingi trilioni 3.5 zimepokelewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali.
Akizungumza leo Julai 20,2025 na waandishi wa habari jijini Dodoma , Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Kenani Laban Kihongosi amesema fedha hizo zimetekeleza miradi ya maendeleo katika sekta za utawala bora (Sh bilioni 958.6), afya (bilioni 94.2), elimu (bilioni 267), maji (bilioni 686.9), barabara (bilioni 638.9), nishati (bilioni 99.2), mapato ya ndani (bilioni 240.9), TASAF (bilioni 61.6), huku sekta nyingine zikitengewa Sh bilioni 465.39.
AFYA: Idadi ya Vituo Yapanuka, Vifo vya Mama na Mtoto Vyashuka
Kihongosi amesema vituo vya kutolea huduma za afya vimeongezeka kutoka 249 hadi 350. Hospitali mpya 8, zahanati 38 na huduma 11 za kibingwa zimeanzishwa zikiwemo huduma za figo, saratani, mifupa na afya ya mama na mtoto. Vifo vya wajawazito vimepungua kwa asilimia 78 kutoka 50 hadi 11, huku vifo vya watoto chini ya miaka mitano vikishuka kutoka 859 hadi 117 sawa na punguzo la asilimia 86.4.

ELIMU: Shule Mpya, Mabweni, Maabara na TEHAMA
Sh bilioni 267 zimetumika katika sekta ya elimu ambapo bilioni 98.9 ziliboresha miundombinu. Shule mpya 27 za sekondari, saba za msingi, madarasa 843, mabweni 60, maabara 78, maktaba 26 na majengo 26 ya TEHAMA yamejengwa. Idadi ya wanafunzi wa elimu bila malipo imeongezeka kutoka 390,910 hadi 430,511. Shule za mahitaji maalum zimeongezeka kutoka 38 hadi 149.
MAJI: Huduma Yafikia 99% Mjini, 77.3% Vijijini
Sh bilioni 686.9 zimetumika katika sekta ya maji kupitia AUWSA (bilioni 568.4) na RUWASA (bilioni 118.5). Mradi mkubwa wa maji Jiji la Arusha umeongeza uzalishaji kutoka lita milioni 60 hadi milioni 200 kwa siku, na huduma ya maji mjini kufikia asilimia 99. Vijijini, miradi 72 imekamilika na vijiji vyenye huduma ya maji vimefikia 351, huku uzalishaji ukifika lita milioni 58.4 kwa siku.
MIUNDOMBINU: Lami, Madaraja na Barabara za Kisasa
Sh bilioni 635.8 zimetumika kupitia TANROADS na TARURA. Barabara za lami zimefikia km 479.88, makalvati yameongezeka kutoka 870 hadi 1,650, na madaraja kutoka 90 hadi 144. Usanifu wa barabara mpya zinazounganisha Arusha na Longido, Kisongo na Namanga unaendelea.
NISHATI: Umeme Wakifikia Vijiji Vyote
Kwa kutumia Sh bilioni 117.739, TANESCO na REA wametekeleza miradi ya nishati ambapo vijiji vyote 368 vya Arusha vina umeme, wateja 306,674 wameunganishwa. Kituo cha kupoza umeme cha Lemugur (MW 250) kimekamilika na mradi wa kuunganisha gridi ya Tanzania na Kenya kupitia Namanga unaendelea.
KILIMO NA MIFUGO: Umwagiliaji, Mazao Yaongezeka
Sh bilioni 85.2 zimetolewa kwa kilimo na bilioni 1.5 kwa mifugo. Mradi wa umwagiliaji Eyasi (hekta 5,000) unatekelezwa Karatu kwa bilioni 38.4 ukiwanufaisha wakulima 3,000. Uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka kutoka tani 450,015 hadi tani 536,581.
UWEZESHAJI WANANCHI: Mikopo, Ajira na TASAF
Mikopo ya asilimia 10 imeongezeka kutoka Sh bilioni 3.08 hadi bilioni 13.55. Vikundi vya walengwa vimeongezeka kutoka 721 hadi 1,380. TASAF imetoa Sh bilioni 57.22 kwa kaya masikini, na mapato ya ndani ya Halmashauri yameongezeka kutoka bilioni 34.6 hadi 110.1, sawa na ongezeko la asilimia 318.
UTALII NA USAFIRI WA ANGA: Filamu ya Royal Tour Yavutia Uwekezaji
Kupitia mchango wa filamu ya Royal Tour ya Rais Samia, Arusha imepokea Sh bilioni 103 kuboresha viwanja vya ndege vya Arusha (Kisongo) na Manyara. Uwanja wa Arusha sasa ni wa pili kwa miruko nchini. Serikali imetenga Sh bilioni 11 kuwezesha operesheni za ndege za kimataifa saa 24. Makumbusho ya Jiolojia ya Kisasa Ngorongoro yajengwa kwa Sh bilioni 25 kwa ushirikiano na China.
MICHEZO: Uwanja wa AFCON 2027 Waendelea Kujengwa
Sh bilioni 298 zimetumika kujenga Uwanja wa Mpira wa Miguu wa SAMIA SULUHU AFCON ARUSHA, kwa ajili ya mashindano ya AFCON 2027. Hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 44.2.

No comments:
Post a Comment