Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) ni miongoni mwa taasisi, kampuni, mashirika ya umma na binafsi pamoja na wajasiriamali wanaoshiriki katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Sabasaba jijini Dar es Salaam.
Katika maonesho hayo, TTCL imejipambanua kama muunganishaji mahiri na suluhisho la kuaminika katika sekta ya TEHAMA, likijivunia kutoa huduma salama, za kisasa na zinazojibu mahitaji halisi ya taasisi za umma, mashirika binafsi na wananchi wa kawaida.
Akizungumza katika banda la TTCL namba 26, Meneja wa Banda, Bi. Janeth Maeda, amewataka Watanzania na washiriki wote wa maonesho hayo kutembelea banda hilo ili kujionea huduma bunifu zinazolenga kuongeza ufanisi na usalama wa taarifa.
“TTCL ni suluhisho la sasa na la baadaye katika huduma za TEHAMA. Tumeaminiwa na Serikali kusimamia miundombinu ya kimkakati kama Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) na Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data Kimtandao (NIDC),” amesema Bi. Maeda.
Amesema TTCL inahudumia taasisi nyingi za umma na binafsi, zikiwemo wizara zote, taasisi za fedha, sekta ya afya, elimu, usafirishaji, utalii, madini na mashirika yasiyo ya kiserikali, kwa kutumia teknolojia ya fiber optic yenye kasi na usalama wa hali ya juu.
Kwa mujibu wa Maeda, huduma za TTCL zimechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za mawasiliano, kuimarisha usalama wa taarifa na kuongeza ufanisi wa taasisi hizo katika kuwahudumia wananchi.
“Kupitia huduma zetu za uhifadhi salama wa taarifa (Data Center), mawasiliano ya ndani ya nchi, na mifumo ya TEHAMA, taasisi mbalimbali zimepiga hatua kubwa kimaendeleo,” aliongeza Maeda.
Aidha, TTCL inatoa punguzo maalum katika msimu huu wa sabasaba kwa vifaa vya mobile broadband kama vile Routers, USB Modems na MIFI, ili kuwawezesha wananchi kumiliki vifaa vya kisasa kwa gharama nafuu na kufurahia huduma bora za mawasiliano.
Bi. Maeda amewaasa wananchi, kampuni, taasisi na wadau wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi kutembelea banda hilo kujifunza namna ya kuboresha shughuli zao kwa kutumia huduma za kidigitali zinazotolewa na TTCL.
No comments:
Post a Comment