
Na Mwandishi Wetu, Singida
Wimbi la matumaini limezidi kuongezeka miongoni mwa wachimbaji wadogo wa madini ya shaba katika kata ya Ibaga, wilaya ya Mkalama mkoani Singida, baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuridhia utolewaji wa vibali vya uchimbaji katika maeneo yao.
Hatua hiyo imeibua mwamko mpya wa kiuchumi kwa vijana na wanawake waliokuwa hawana ajira, huku wengi wakieleza jinsi uchimbaji wa shaba ulivyobadilisha maisha yao kutoka hali ya utegemezi hadi kuwa wajasiriamali waliowekeza kwenye kilimo, elimu, na makazi bora.
“Elimu tuliyopata kuhusu uchimbaji salama imeleta mabadiliko makubwa. Tunafanya kazi kwa tija, kwa usalama, na kwa mujibu wa sheria,” amesema Elvis Jeremiah, mmoja wa wachimbaji wa shaba kutoka Ibaga. Ameongeza kuwa kurejea kwa viwanda vya usafishaji wa shaba nchini kumeimarisha masoko na kuongeza thamani ya madini hayo.
Miongoni mwa viwanda vilivyotajwa kuleta mabadiliko hayo ni Shengde Precious Metal Resources cha Dodoma na Mineral Access Systems Tanzania Ltd (MAST) cha Mbeya, ambavyo vimesaidia kuvutia wanunuzi na kuongeza ajira kupitia minyororo ya uchenjuaji na usafirishaji wa madini.
Kwa upande wake, Frank Saila kutoka tarafa ya Kirumi ametoa ushuhuda wa mafanikio aliyoyapata kupitia uchimbaji. “Nimenunua pikipiki, ujenzi wa nyumba yangu, kusomesha watoto na kuihudumia familia yangu. Maisha yamebadilika kabisa,” amesema.
Aidha, wachimbaji hao wameishukuru Serikali kwa kuwapatia mafunzo ya usalama kazini, kulinda afya na mazingira, na namna ya kupata leseni halali, jambo ambalo limewasaidia kufanya kazi kwa uaminifu na ufanisi.
Wakati wakitoa shukrani zao, wachimbaji hao pia wameiomba Serikali kupitia Tume ya Madini kusaidia upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya uchimbaji madini ili kuimarisha zaidi uzalishaji, kuongeza mapato ya Serikali na kuchochea ajira kwa vijana wengi zaidi.
“Tuna matumaini kuwa kupitia uongozi thabiti wa Mhe. Rais Samia, sekta ya madini itaendelea kuwa kichocheo cha maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla,” amehitimisha Jeremiah.










No comments:
Post a Comment