
Wizara ya Afya,Idara ya Kinga ya Kinga, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma imeandaa kikao kazi maalum cha kuhuisha vielelezo vya kuelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu magonjwa ya mlipuko pamoja na magonjwa mengine mbalimbali yanayoathiri jamii.
Kikao hiki kimefanyika mkoani Morogoro katika Ukumbi wa Chuo cha Masafa kikiwakutanisha wataalamu mbalimbali wa afya kutoka Wizara ya Afya na taasisi za afya kwa lengo la kufanya uhakiki wa mwisho (validation) wa vifaa vya mawasiliano vya afya kwa jamii (IEC/SBCC materials) vilivyoandaliwa kufuatia tathmini ya mwenendo wa magonjwa nchini, iliyotolewa na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Serikali.
Akifungua kikao hicho, Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma kutoka Wizara ya Afya Dkt. Ona Machangu amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha vielelezo vya elimu ya afya na kuhakikisha vinakuwa vya kisasa na vleweka kirahisi, vinavyohusisha jamii, na vinavyoendana na tamaduni za Watanzania ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu magonjwa ya mlipuko kama vile Mpox, Kipindupindu, Dengue, Surua, usafi wa mazingira (WASH).
“Tuna wajibu wa kuhakikisha kila ujumbe unaotolewa kwa jamii unakuwa sahihi, unaeleweka kwa haraka, na unaamsha hatua chanya. Kazi yetu hapa ni kuhakikisha nyenzo hizi zinafikia viwango bora kabla ya kuanza kusambazwa,” amesema Dkt. Machangu.
Katika kikao hiki, washiriki wanapitia kwa makini vielelezo mbalimbali vikiwemo:Mabango (posters), Vipeperushi (brochures)
, Matanagazo ya redio na televisheni (radio & TV spots)
na Machapisho ya kidigitali kwa mitandao ya kijamii (digital flyers).
Vielelezo hivyo vimetengenezwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo wawakilishi wa watu wanaoishi na VVU (PLHIV) ili kuhakikisha vinazingatia ujumuishaji, kupunguza unyanyapaa, na kuhamasisha tabia bora za afya.
Maudhui haya pia yanahamasisha matumizi ya Afya Call Centre (199) kama chanzo cha taarifa sahihi za kiafya nchini.
Baada ya kikao hiki, timu ya wataalamu kutoka Sehemu ya Elimu ya Afya Kwa Umma itayapitia tena mapendekezo yote yaliyotolewa na kuyafanyia kazi kwa ajili ya kufanya marekebisho ya mwisho kabla ya kusambazwa kitaifa kupitia vyombo vya habari, vituo vya afya, mitandao ya kijamii, shuleni, taasisi za dini, na jamii kwa ujumla.
Wito umetolewa kwa washiriki wote kutoa maoni ya kina kuhusu kila kielelezo ili kuhakikisha nyenzo hizo zinafikia kiwango cha ubora wa juu na kuwa na athari chanya kwa jamii.








No comments:
Post a Comment