WATAKAOSOMEA FANI ZA SAYANSI ZA DATA, AKILI UNDE NA SAYANSI SHIRIKISHI KUFADHILIWA NA SERIKALI - PROF. MKENDA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, July 8, 2025

WATAKAOSOMEA FANI ZA SAYANSI ZA DATA, AKILI UNDE NA SAYANSI SHIRIKISHI KUFADHILIWA NA SERIKALI - PROF. MKENDA


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amezindua rasmi programu ya Samia Extended Scholarship DS/A+, inayolenga kufadhili wanafunzi wa Tanzania bara na Zanzibar kusoma katika vyuo vikuu mahiri duniani katika fani za kimkakati za Sayansi ya Data, Akili Unde (Artificial Intelligence), na Sayansi Shirikishi kwa mwaka wa masomo 2025/2027.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika Julai 8, 2025 jijini Arusha, Prof. Mkenda alieleza kuwa mpango huo unalenga kuwanufaisha wanafunzi 50 waliobobea katika tahasusi za sayansi asilia zenye hisabati ya juu (advanced mathematics). Alibainisha kuwa waombaji watakaofanikiwa watahitajika kushiriki Kambi ya Kitaifa ya Maarifa kwa muda wa miezi kumi (10) katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) kabla ya kuanza masomo yao nje ya nchi.

Prof. Mkenda alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga kuwekeza kwa dhati katika maendeleo ya sayansi, teknolojia na ubunifu kwa ajili ya maendeleo ya taifa. Alitoa wito kwa vijana kutumia fursa hiyo kwa bidii na maarifa ili kuchochea mageuzi ya kisayansi na kiteknolojia nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu, amesema Programu ya Samia Extended Scholarship (DS/A+) inatekelezwa kwa hatua tatu, ambapo ya kwanza inahusisha kambi ya kitaifa ya maarifa kwa miezi kumi ili kuwapa vijana mafunzo ya uzalendo, maadili ya kitaifa na mawasiliano ya kimataifa.

Akizungumza Julai 8, 2025 jijini Arusha wakati wa uzinduzi wa programu hiyo, Dkt. Nungu alieleza kuwa hatua ya pili ni maandalizi ya kisaikolojia kwa vijana kabla ya kusoma nje ya nchi, huku hatua ya tatu ikitoa ufadhili wa masomo ya Uzamili katika Sayansi ya Data na Akili Unde kupitia ushirikiano na Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela NM-AIST
na IIT Madras Zanzibar.

Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Programu hiyo, Prof. Makenya Maboko, ameishukuru Serikali kwa kuanzisha mpango huo unaowawezesha vijana wa Kitanzania kujifunza taaluma za sayansi kama data, hatua ambayo itaisaidia nchi kuendana na maendeleo ya teknolojia na kukuza uchumi.

Makamu Mkuu wa Taasisi ya NM-AIST, Prof. Maulilio Kipanyula, amesema taasisi yao imejiandaa kikamilifu kutoa mazingira bora ya mafunzo ili kuwajengea wanufaika maarifa na ujuzi wa kisasa.








No comments:

Post a Comment