Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Karagwe kimetangaza matokeo rasmi ya kura za maoni za kumpata mgombea wa Ubunge wa Jimbo la Karagwe kupitia CCM, kufuatia uchaguzi uliofanyika tarehe 04 Agosti 2025.
Katika matokeo hayo, Ndugu Innocent Lugha Bashungwa ameibuka mshindi kwa kupata kura 7,902, akiwapiku kwa mbali wagombea wengine watano waliokuwa wakiwania nafasi hiyo.
Matokeo kamili ni kama ifuatavyo:
1. Innocent Lugha BASHUNGWA – Kura 7,902
2. Confort Mugisha BLANDES – Kura 389
3. Princepius Sabinian RWAZO – Kura 381
4. Akida Augustinio MNYAMBO – Kura 113
5. Adolf Andrew LWANTUNGAMO – Kura 110
6. Devotha Obadia ALEXANDA – Kura 13
Matokeo hayo yametangazwa rasmi leo, tarehe 05 Agosti 2025 na Katibu wa CCM Wilaya ya Karagwe, Ndugu Anatory Nshange, mbele ya Wagombea, Wanachama na viongozi wa chama waliokusanyika kushuhudia hatua hiyo muhimu katika mchakato wa kuelekea uchaguzi mkuu.
Nshange ameeleza kuwa Katika mchakato huo jumla ya wajumbe waliopiga kura walikuwa 8,969, ambapo kura halali zilikuwa 8,908 na kura 61 ziliharibika.
Aidha, wagombea wengine wamempongeza mshindi wa kura hizo Ndugu Bashungwa kwa ushindi wake wa kishindo. Wameeleza kuwa mchakato mzima wa uchaguzi wa kura za maoni umeendeshwa kwa uwazi, haki na uaminifu mkubwa, na wameahidi kuendelea kushirikiana na chama kwa ajili ya ustawi wa Jimbo la Karagwe na ushindi wa CCM katika Uchaguzi Mkuu ujao.
No comments:
Post a Comment