Naibu Waziri wa Madini Mhe. Dkt. Steven Kiruswa ametoa wito kwa timu ya waokoaji kuongeza kasi na juhudi katika shughuli za uokoaji wa wachimbaji wadogo wa madini waliopata ajali ya kukwama chini ya ardhi, kufuatia kutitia kwa mgodi na kuporomoka kwa kifusi katika mgodi wa dhahabu wa Nyandolwa unaomilikiwa na kikundi cha Wachapakazi, uliopo katika kijiji cha Mwongozo, Kata ya Mwenge, Halmashauri ya Shinyanga, mkoani Shinyanga.
Akizungumza baada ya kutembelea eneo la tukio, Dkt Kiruswa amesema serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu juhudi za uokoaji huku akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa maisha ya wachimbaji waliokwama chini ya mgodi yanapewa kipaumbele kupitia juhudi za haraka na za kitaalamu.
Aidha, amesema, katika ajali hiyo, wachimbaji wapatao 25 walikwama chini ya ardhi kufuatia kutitia kwa mgodi na kuporomoka kwa kifusi Agosti 11, 2025. Hadi sasa, taarifa zinaeleza kuwa watu wanne wameokolewa wakiwa hai na kati yao mmoja amefariki wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Wilaya ya Shinyanga, juhudi za kuwaokoa wengine zinaendelea.
"Tunaendelea kushirikiana na vyombo vya uokoaji, ikiwemo Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, wataalamu wa madini, pamoja na wanajamii, kuhakikisha tunawafikia waliobaki kwa haraka iwezekanavyo," amesema Dkt. Kiruswa.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kiruswa ametoa pole kwa familia za waathirika wa ajali hiyo na kuwataka wachimbaji wadogo kufuata taratibu na kanuni za usalama katika shughuli za uchimbaji ili kuepuka ajali za aina hiyo siku zijazo.
Serikali imeahidi kuendelea kutoa msaada wa kiufundi na vifaa ili kurahisisha kazi ya uokoaji na kuhakikisha shughuli hiyo inatekelezwa kwa ufanisi na usalama.
Kwa upande wake, Mkaguzi MkuuwaMigodikutokaTume ya Madini Mhandisi Khamisi Kamando, amesema ajali hiyo ilitokea majira ya asubuhi wakati wakiwa kwenye shughuli za ukarabati wa mashimo (maduara) matatu tofauti ambapo yalititia wakati wachimbaji hao wakiwa chini ya ardhi.
Pia, Timu ya uokoaji kutoka mgodi wa uchimbaji mkubwa wa madini ya dhahabu wa Barrick Bulyanhulu Gold Mining umefika katika eneo la tukio kwa ajili ya kuongeza nguvu katika zoezi la uokoaji.
No comments:
Post a Comment