
Na Anangisye Mwateba, Kigoma
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula, amelielekeza Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kuandaa mpango mkakati wa kutangaza vivutio vya kipekee vya utalii, hususan katika hifadhi za kimkakati kama Hifadhi ya Taifa ya Gombe.
Akizungumza Agosti 18, 2025, wakati wa ziara yake katika Hifadhi hiyo, Mhe. Kitandula amesema Gombe inajivunia vivutio vya kipekee duniani, vikiwamo wanyama watatu walioko hatarini kutoweka Sokwe mtu, Mbega mwekundu na Kakakuona ambao ni hazina adimu ya taifa.
“Mpango huu wa utangazaji uandaliwe na kitengo cha masoko cha TANAPA kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) pamoja na waongoza watalii ili kuhakikisha vivutio hivi vinapata uhamasishaji unaostahili katika soko la ndani na nje ya nchi,” amesema Kitandula.
Amebainisha kuwa Hifadhi ya Gombe ni maarufu kimataifa kwa kuwa na Sokwe mtu, jambo linaloweza kuimarisha zaidi sekta ya utalii iwapo litapewa uzito wa kipekee kwenye mikakati ya utangazaji.
“Niwapongeze wahifadhi wa Gombe kwa kazi kubwa mnayofanya ya kulinda viumbe walioko hatarini. Hii ni ishara ya kizalendo kwa taifa na kwa rasilimali zetu za asili. Ni wajibu wetu kuhakikisha sekta ya utalii inaendelea kuchangia pato la taifa,” amesisitiza.
Hifadhi ya Taifa ya Gombe pia ni maarufu kutokana na utafiti wa muda mrefu uliofanywa na mtafiti wa Kiingereza, Jane Goodall, aliyewasili Julai 14, 1960 akiwa na mama yake, kwa ajili ya kuchunguza maisha ya Sokwe mtu. Utafiti huo umechangia kwa kiasi kikubwa katika maarifa ya kisayansi kuhusu mnyama huyo kwa zaidi ya miaka 60 sasa.
Katika ziara hiyo, Mhe. Kitandula pia alitembelea makumbusho ya Dkt. David Livingstone yaliyopo katika Manispaa ya Kigoma Ujiji.








No comments:
Post a Comment