MAKANDARASI WANAWAKE WATAKIWA KUTEKELEZA MIRADI YA BARABARA KWA UFANISI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, August 7, 2025

MAKANDARASI WANAWAKE WATAKIWA KUTEKELEZA MIRADI YA BARABARA KWA UFANISI


Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi imetoa rai kwa Makampuni 15 ya Makandarasi Wanawake waliopata fursa ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilometa 20 katika barabara ya Ruanda - Idiwili Mkoani Songwe kuutekeleza mradi huo ipasavyo kwa ubora, uaminifu na muda uliopangwa.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Barabara kutoka Wizara ya Ujenzi Mhandisi Alois Matei wakati akimwakilisha Katibu Mkuu Balozi Mhandisi Aisha Amour katika ufunguzi wa Kongamano la Tano la Makandarasi Wanawake lililofanyika leo Agosti 07, 2025 jijini Dar es Salaam.

“Mafanikio ya mradi huu wa barabara ambao mmepewa na Serikali wa majaribio utafungua milango kwa miradi mingine zaidi ili Makandarasi  Wanawake wengine pia wapate fursa hizo”, amesisitiza Mhandisi Matei.

Ameongeza kuwa Serikali imepanua wigo wa thamani ya miradi inayotolewa kwa Makandarasi Wazawa hadi kufikia Bilioni 50 ikiwa ni hatua muhimu ya kuweza kushiriki miradi mikubwa ya maendeleo inayoendelea hapa nchini na kusisitiza kwa Makandarasi Wazawa wote kuzichangamkia fursa za miradi hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Matangenezo ya Barabara kutoka TANROADS, Mhandisi Dkt. Christina Kayoza ameeleza Serikali inaendelea kukuza Makandarasi Wazawa nchini hivyo amewataka Makandarasi Wanawake kuzitumia fursa hizo wanazopata za utekelezaji wa miradi kuzitumia vizuri kwa kudumisha mshikamano ili waweze kufika mbali na pia kama TANROADS itaendelea kushirikiana na Makandarasi hao bega kwa bega.

Naye, Rais wa Chama cha Makandarasi Wanawake Tanzania  (TWCA) Mhandisi Judith Odunga ametaja kuwa katika kipindi cha miaka mitano Chama kimepata mafanikio mengi ikiwemo Makandarasi Wanawake kupewa kazi nyingi za ujenzi wa barabara kwa class V hadi VII  pamoja na kazi za Labour based kupitia Taasisi za TARURA, TANROADS na nyinginezo.

“Tunaishukuru Serikali kwani kupitia Mawakala wake wa barabara imeendelea kutangaza miradi maalum kwa ajili ya kampuni za wanawake pekee ambapo ushindani unafanyika miongoni mwetu tu”, ameeleza Mhandisi Odunga.

Chama cha Makandarasi Wanawake Tanzania kimesajiliwa kwa lengo la kuwaleta pamoja Wakandarasi Wanawake ili kuwajengea uwezo kupitia mafunzo mbalimbali na kuongeza ufanisi wa biashara zao, kuwa na sauti ya pamoja katika kusimamia utekelezaji wa fursa mbalimbali zinazowahusu Makandarasi Wanawake.


No comments:

Post a Comment