Mgombea Uraisi wa Shirikisho la Riadha Tanzania (SRT) Bw. Nsolo Malongo Mlozi ameahidi mabadiliko chanya kwenye mchezo wa riadha. Riadha ni mchezo unaochezwa uwanjani (mbio fupi, tufe na mkuki) na barabarani (mbio za kati na ndefu) ambao umekuwa unaiweka taswira ya nchi kimataifa tangu miaka ya nyuma.
Nsolo ni mtaaluma kwenye ukaguzi wa mahesabu, fedha, biashara na uchumi kilimo kwa takribani miaka 19. Kwenye riadha amekuwa mdau mkubwa na muandaaji wa mbio mbalimbali ikiwemo mbio ambayo yeye ni Mkurugenzi ya Capital City Half Marathon inayofanyika Jijini Dodoma kwa miaka 7 mfululizo tangu 2019 ambayo inatumia mtambo maalum wa kuongozea mbio (Race Timing System) unaomilikiwa na kampuni yake.
Sambamba na hilo Nsolo ni mwalimu wa riadha ambae amepata cheti toka SRT na mkimbiaji wa kitaifa (takribani mbio zote Tanzania Bara na Visiwani) na kimataifa umbali wa 42.2km (ikiwemo Kilimanjaro Marathon (2019-2025), Nairobi Marathon (2020-2022), Dubai Marathon (2023), Capetown Marathon (2023) na Berlin Marathon (2024). Mbio ya Berlin Marathon ni moja ya mbio 7 kubwa duniani (The Abbort World Marathon Majors) ambayo alishiriki na kuvunja rekodi yake binafsi.
Nsolo ameainisha vipaumbele vyake kama akipata ridhaa ya kuwa Rais wa SRT ikiwemo;
- Kudumisha mashirikiano na mahusiano (viongozi wenzangu, vyama vya Mikoa/Wilaya, Serikali, Baraza, Taasisi, Wadhamini, Wachezaji, Wadau, Klabu, Makocha, Walimu na waandishi wa habari).
- Kuleta maendeleo na kuinua mchezo ikiwemo kusomesha walimu, makocha, wachezaji, wataalamu kwa kutafuta wadau wa kushirikiana na SRT.
- Kupanua wigo wa uwekezaji (viwanja, wachezaji, vifaa, nk) na udhamini kwenye riadha kuanzia ngazi za wilaya, mikoa, Taifa na kimataifa ili kuhakikisha tunapata wachezaji waliobora na walioshindanishwa.
- Kuunda mifumo sahihi ya uongozi ikiwemo mabadiliko ya teknolojia wezeshi kuhakikisha tunaongoza kwa tija na kuwa na kanzi data sahihi.
- Mabadiliko ya katiba na kanuni zinazoendana na hali ya sasa pale itakapohitajika.
- Kutafuta vyanzo vingine vya mapato ikiwemo kuwa na mikataba sahihi ya udhamini itakayowezesha SRT na vyama kujiendesha ikiwemo ofisi, mali, samani, nk. Sambamba na hili kuwa na mfumo sahihi wa kujadili mapato na matumizi na kuweka mkaguzi wa mahesabu ili kusimamia matumizi sahihi ya fedha.
No comments:
Post a Comment