Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Patrick Allute (aliyenyoosha mkono) akisisitiza jambo wakati akikagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa makazi ya Watumishi wa Umma unaojengwa katika Kijiji cha Maluga, Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, mkoani Singida. Wengine ni maafisa kutoka Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Wizara ya Fedha na Watumishi Housing Investments.
Na. Veronica Mwafisi-Singida
Timu ya wataalam kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Wizara ya Fedha na Watumishi Housing Investments ikiongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Bw. Patrick Allute imekagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa makazi ya Watumishi wa Umma kwa upande wa elimu yanayojengwa katika Kijiji cha Maluga, Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, mkoani Singida uliofikia 70% ambapo ukikamilika rasmi utawasaidia watumishi hao kuwa karibu na ofisi wanazofanyia kazi kwa lengo la kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Mara baada ya kukagua mradi huo leo, Kaimu Mkurugenzi Allute amesema, kuna umuhimu wa makazi ya watumishi wa umma kuwa karibu na ofisi kwani itaongeza tija ya utendajikazi serikalini.
“ujenzi huu wa makazi ya watumishi wa umma una umuhimu sana kwani utasaidia kuongeza utendajikazi kwa watumishi wa eneo hili, lakini pia utasaidia kuepeukana na changamoto ya makazi ambayo imekuwa ikiwakabili watumishi hao na kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi,” amesema Mkurugenzi Allute
Vilevile, timu hiyo imekagua maendeleo ya ujenzi wa makazi ya watumishi wa umma kwa upande wa afya katika Kijiji cha Makunda Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, mkoani Singida.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Mipango na Bajeti, Bi. Julieth Magambo amewasisitiza Watumishi Housing Investments (WHI) ambao ndio kandarasi inayojenga makazi katika mradi huo kuhakikisha wanakamilisha miradi hiyo kwa wakati ili kuendana na mipango na bajeti ya Serikali.
Naye, Mhandisi Salum Chanzi kutoka WHI, ameahidi kukamilika kwa wakati mradi huo ili kufikia malengo ya Serikali katika kuwatengenezea mazingira bora watumishi wa umma.
Kwa upande wake, Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya fedha, Bw. Ezekiel Odipo ameeleza kuwa, Serikali inatoa fedha nyingi ili kutimiza malengo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuongeza tija kwa watumishi wa umma ili waweze kutoa huduma bora kwa maendeleo ya taifa.
Mradi wa ujenzi wa makazi hayo ya watumishi wa umma upo katika hatua ya majaribio ambayo unatekelezwa kwenye mikoa ya Dodoma, Lindi, Singida, Pwani na Ruvuma.
No comments:
Post a Comment