WAZIRI MKENDA AWATAKA VIJANA KUSIMAMIA KWA UWAZI NA UWADILIFU RASILIMALI ZA UMMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, August 15, 2025

WAZIRI MKENDA AWATAKA VIJANA KUSIMAMIA KWA UWAZI NA UWADILIFU RASILIMALI ZA UMMA



Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amewataka vijana nchini kuwajibika kikamilifu katika kusimamia matumizi sahihi ya rasilimali za umma, sambamba na kupinga vitendo vya rushwa.

Akizungumza 14 Agosti 2025 jijini Arusha wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la Uwajibikaji kwa Vijana 2025 linaloandaliwa na Youth Accountability Initiative Forum (YAIF), Prof. Mkenda amesema kuwa rushwa ni miongoni mwa vikwazo vikubwa vinavyorudisha nyuma maendeleo ya taifa, na kwamba vijana wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuikataa na kuikemea.

"Uwajibikaji si jukumu la viongozi pekee, bali ni wajibu wa kila Mtanzania, hususan vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa,” alisema Waziri Mkenda.

Aimepongeza YAIF kwa kuratibu jukwaa hilo lenye dhamira ya kuwahamasisha vijana kushiriki katika mijadala ya uwajibikaji, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kujenga kizazi chenye maadili, uzalendo, na uelewa wa masuala ya utawala bora.

Prof. Mkenda pia aliwapongeza washiriki wa shindano la uandishi wa insha lililobeba maudhui ya *“The Role of Public Accountability in the Proper Management of Public Resources”*, pamoja na Klabu Bora ya Mwaka 2024/2025 kwa mchango wake katika kusukuma mbele ajenda ya uwajibikaji kwa vijana.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Wajibu, FCPA. Ludovick Utouh, ameeleza kuwa ushiriki wa vijana ni nguzo muhimu katika kuhakikisha rasilimali za umma zinasimamiwa kwa uadilifu, uwazi na kwa manufaa ya wote, na kwamba taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na wadau wengine kuimarisha misingi ya uwajibikaji nchini.

Jukwaa hilo limehudhuriwa na vijana kutoka mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara, na limejikita katika kuendeleza mijadala ya uwajibikaji, uwazi, na uadilifu katika matumizi ya rasilimali za umma.


No comments:

Post a Comment