MWENYEKITI WA TUME YA MADINI ATEMBELEA BANDA LA TUME KWENYE MAONESHO YA NANENANE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, August 7, 2025

MWENYEKITI WA TUME YA MADINI ATEMBELEA BANDA LA TUME KWENYE MAONESHO YA NANENANE



Dodoma, Agosti 7, 2025


Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet R. Lekashingo, ameongoza ujumbe wa Tume kutembelea Banda la Tume ya Madini katika Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima (Nane Nane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.

Dkt. Lekashingo ameambatana na Makamishna wa Tume, Mhandisi Theonestina Mwasha na Dkt. Theresia Numbi, pamoja na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo. 

Wakiwa katika banda hilo, wamepata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Tume, ikiwemo utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu fursa za uwekezaji katika Sekta ya Madini, taratibu za upatikanaji wa leseni, biashara ya madini, uongezaji thamani madini, pamoja na usimamizi wa mazingira katika shughuli za uchimbaji.

Akizungumza na maafisa wa Tume na wananchi waliotembelea banda hilo, Dkt. Lekashingo amewapongeza watumishi wa Tume kwa kazi nzuri ya kutoa elimu na huduma kwa umma. 


Amesisitiza umuhimu wa kutumia maonesho hayo kama jukwaa la kuelimisha na kuhamasisha Watanzania kushiriki kikamilifu katika Sekta ya Madini, hususan kupitia uongezaji thamani madini na kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyopo.

“Ni muhimu wananchi wakapata uelewa mpana kuhusu namna wanavyoweza kunufaika na rasilimali za madini zilizopo nchini iwe ni kupitia uchimbaji, biashara, uongezaji thamani au utoaji wa huduma kwenye migodi. Sekta hii ina mchango mkubwa katika Pato la Taifa na ajira kwa Watanzania,” amesisitiza Dkt. Lekashingo.

Kwa upande wao, Makamishna wa Tume wameeleza kufurahishwa na mwitikio mkubwa wa wananchi kutembelea banda la Tume na kuonesha dhamira ya kujifunza zaidi kuhusu Sekta ya Madini, jambo linalodhihirisha hamasa na mwamko chanya wa Watanzania kushiriki kwenye sekta hiyo muhimu.

Naye Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, amewataka maafisa wa Tume kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kulingana na mahitaji ya wadau waliopo katika maonesho mbalimbali nchini.

“Yapo madini yanayotumika kama mbolea, na pia zipo fursa nyingi za usambazaji wa bidhaa za kilimo kwenye migodi. Ni muhimu wananchi wakafahamu fursa hizi na kushiriki kikamilifu ili Sekta ya Madini iendelee kuwa kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi na mchango wake katika Pato la Taifa uongezeke,” amesema Mhandisi Lwamo.

Tume ya Madini ni miongoni mwa Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Madini zinazoshiriki kikamilifu katika Maonesho ya Nane Nane mwaka huu, ikiwa na lengo la kuelimisha umma kuhusu Sekta ya Madini, kuonesha mafanikio yaliyopatikana, pamoja na kuhamasisha uwekezaji zaidi katika sekta hiyo kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

No comments:

Post a Comment